Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei ametoa wito kwa mataifa ya Kiislamu yenye uhusiano wa kisiasa na Israel kukata mahusiano kwa kipindi fulani, vyombo vya habari vya kitaifa vimeripoti Jumapili, ikiwa ni wiki kadhaa baada ya kutoa wito wa vikwazo vya mafuta na chakula dhidi ya Israel.
Baadhi ya serikali za Kiislamu zimelaani uhalifu wa Israel katika mikutano mbali mbali wakati baadhi yao hawajafanya hivyo. Hili halikubaliki, alisema Khamenei kabla ya kusisitiza kuwa jukumu kuu la serikali za Kiislamu ni kusitisha nishati na bidhaa nyingine kwenda Israel. Serikali za Kiislamu zinapaswa angalau kusitisha uhusiano wa kisiasa na Israel kwa muda kadhaa, alisema Khamenei.
Wakati wa mkutano wa pamoja kati ya wanachama wa Umoja wa nchi za Kiislamu na Umoja wa Nchi za Kiarabu katika mji mkuu wa Saudi Arabia hapo Novemba 11, mataifa ya Kiislamu hayajakubali kuiwekea Israel vikwazo vingi, kama ilivyoombwa na Rais wa Iran Ebrahim Raisi.