Mbunge mmoja wa zamani nchini Misri, Ahmed al-Tantawi amesema Jumamosi kwamba anachelewesha kurejea nyumbani Misri kutoka Lebanon kufuatia kukamatwa kwa watu 12 walio karibu naye baada ya yeye kutangaza azma ya kugombea urais.
Tantawi mkosoaji mkubwa wa Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi alikimbia Misri mwaka 2022 kufuatia ripoti katika vyombo vya habari kwamba alikabiliwa na vitisho vya usalama. Alitarajiwa kurudi nyumbani kutoka Lebanon siku ya Jumamosi lakini alitangaza katika ujumbe wa Facebook kuwa safari yake itacheleweshwa hadi siku nyingine ambayo haikutajwa ndani ya kipindi cha wiki moja.
Mwezi Machi, Tantawi alitangaza kurejea Misri na alipanga kugombea urais ili kutoa njia ya kidemokrasia kwa utawala uliopo sasa madarakani. Human Rights Watch, siku ya Ijumaa walisema angalau wanafamilia kumi na wawili na wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa Tantawi walikamatwa tangu mwishoni mwa April.