Mke wa rais wa zamani wa Marekani Rosalynn Carter alipewa heshima ya mwisho siku ya Jumanne katika ibada maalum huko Atlanta kwenye jimbo la Georgia iliyohudhuriwa na wake wote wa marais walio hai pamoja na marais watatu akiwemo mume wake, Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter mwenye umri wa miaka 99 ambaye aliingia katika huduma maalum ya afya katika dakika za mwisho za uhai hapo mwezi Februari.
Ibada hiyo iliambatana na muziki wa taratibu uliobeba vifungu vya Biblia. Wageni waliokuwepo ni pamoja na Rais Joe Biden na mkewe Jill Biden, Rais wa zamani Bill Clinton na Waziri wa Zamani wa Mambo ya Nje Hillary Clinton, wake wa marais wa zamani Melania Trump, Michelle Obama na Laura Bush wakiambatana na Makamu Rais Kamala Harris na mumewe Doug Emhoff.
Zaidi ya watu 1,000 walihudhuria ibada hiyo wakiwemo watoto wake na darzeni ya wajukuu na vitukuu wakiwa wamekaa mbele na kati-kati karibu na Jimmy Carter.
Carter na mkewe walikuwa wana ndoa kwa miaka 77.