Marekani na Saudi Arabia siku ya Jumapili wamehimza tena haja ya mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya majenerali wa kijeshi wa Sudan wakati mapigano yakiendelea katika wiki yake ya nane.
Makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano yamefikiwa na kuvunjwa, na Marekani iliwawekea vikwazo majenerali wawili wanaohasimiana wiki iliyopita ikizilaumu pande zote mbili kwa umwagaji damu wa kusikitisha.
Wajumbe wa jeshi la Sudan na wanamgambo wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) wamesalia katika mji wa pwani wa Saudi Arabia wa Jeddah licha ya kuvunjika kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano, wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia imesema.
Wapatanishi wa kigeni wametoa wito kwa pande zote kukubaliana na kutekeleza kwa ufanisi usitishaji mpya wa mapigano kwa lengo la kupatikana makubaliano ya kudumu ya kusitisha uhasama, wamesema maafisa mjini Riyadh.