Milipuko na milio ya risasi ilisikika Jumatatu kutoka hoteli moja katika mji mkuu wa Somalia ambayo ilishambuliwa na kundi la waasi siku ya Jumapili.
Watu wanne waliuawa usiku wa kuamkia leo Jumatatu katika hoteli hiyo kulingana na ripoti ya shirika la habari la Agence France Presse (AFP).
"Magaidi wenye silaha wamekwama ndani ya chumba katika jengo hilo na vikosi vya usalama vinakaribia kumaliza tukio hilo hivi karibuni. Kufikia sasa tumethibitisha vifo vya watu wanne," Mohamed Dahir, afisa wa usalama ameliambia shirika la habari la AFP.
Reuters imeripoti kwamba Bunge la Somalia lilifuta vikao vya mabaraza yote ya bunge kutokana na shambulizi la wanamgambo kwenye hoteli.
Wanamgambo wa al-Shabab walifanya shambulizi katika hoteli ya Villa Rays iliyoko katika eneo salama si mbali kutoka ikulu ya rais mjini Mogadishu na gereza linaloendeshwa na idara ya taifa la upelelezi, kwa mujibu wa mashahidi na polisi. Hoteli hiyo hutembelewa na viongozi wa serikali na wanasiasa.
Mashahidi wameviona vikosi maalum vya usalama vikiingia katika eneo hilo. Polisi walisema waliwaokoa raia na maafisa wengi.