Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limepiga kura siku ya Ijumaa kwa idadi ndogo ikiongeza mwaka mwingine kwa tume ya wataalamu iliyopewa jukumu la kuchunguza hali ya haki za binadamu katika eneo lililokumbwa na mzozo nchini Ethiopia.
Waraka uliowasilishwa na Umoja wa Ulaya ulipitishwa kwa kura 21 za kuunga mkono.
Nchi kumi na tisa zilipiga kura dhidi yake, ikiwa ni pamoja na wanachama wote wa Afrika wa Baraza la Haki za Binadamu isipokuwa Malawi ambayo ilijitoa pamoja na nchi nyingine sita.
Wataalamu hao wanatarajiwa kutoa ripoti ya maneno kuhusu hali nchini Ethiopia, ambayo imekumbwa na mzozo tangu Novemba 2020, kwa Baraza la Haki za Binadamu katika kikao chake kijacho mapema mwaka 2023.
Mwakilishi wa Ethiopia mjini Geneva alisema katika ujumbe wa Twitter kabla ya upigaji kura, kwamba "Ethiopia inaikataa kura hiyo na kuwaomba wajumbe wa Baraza hilo kupiga kura dhidi ya mradi huu wa kisiasa".