Mamilioni ya watu barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara wana njaa; inasema ICRC

icrc logo

Kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu inaonya mamilioni ya watu barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara wana njaa kutokana na mizozo, majanga ya hali ya hewa, na kupanda kwa bei za vyakula kwasababu ya uvamizi wa Russia nchini Ukraine.

ICRC inaonya mzozo wa chakula barani Afrika unatarajiwa kuwa mbaya sana. Inasema mizozo na ghasia za silaha, mavuno mabaya kwasababu ya ukame wa miaka mingi, na kuongezeka kwa bei ya chakula na bidhaa nyingine kunawasukuma watu wengi kuingia kwenye umaskini uliokithiri pamoja na njaa.

Tathmini ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa inakadiria watu milioni 346 katika bara hilo wanakabiliwa na uhaba mkubwa sana wa chakula, ikimaanisha kwamba robo moja ya watu hawana chakula cha kutosha.

Mkurugenzi wa ICRC kanda ya Afrika, Patrick Youssef anasema hali ni ya dharura.

Anaonya maisha ya watu wengi yatapotea bila juhudi za pamoja za wadau tofauti kukabiliana na changamoto zilizopo. Anasema mashirika ya misaada, taasisi za kimataifa za fedha, na serikali lazima zishirikiane ili kuzuia mzozo wa kibinadamu usifikie kiwango ambacho hauwezi kubadilishwa.

ICRC inaripoti kuwa vita nchini Ukraine vimesababisha ongezeko kubwa la bei ya mafuta na mbolea. Hiyo inasema imeongeza shinikizo kubwa kwa wakulima ambao wengi wao wanakabiliwa na athari za pamoja za migogoro na majanga ya hali ya hewa.

Youssef anasema pembe ya Afrika imeathirika zaidi. Anaelezea hata hivyo kwamba maeneo mengine ya Afrika, kuanzia Mauritania hadi Sahel, mpaka Ziwa Chad na kwa kiasi kidogo Jamhuri ya Afrika ya kati yanakabiliwa na athari za mgogoro wa Ukraine.