Jumuiya ya kiraia Sudan imekataa pendekezo la Mkuu wa jeshi nchini humo la serikali ya kiraia

Baadhi ya waandamanaji wanaodai kurejeshwa utawala wa kiraia wanaonekana katika mji wa Khartoum, Sudan, July 4, 2022.

Jumuiya kuu ya kiraia nchini Sudan siku ya Jumanne ilikataa pendekezo la kiongozi wa mapinduzi ya nchi hiyo la kutoa nafasi kwa serikali ya kiraia kama njia ya ujanja na kuhimiza maandamano zaidi.

Mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan ambaye unyakuzi wake wa madaraka hapo Oktoba mwaka 2021 ulizuia mpito kwa utawala wa kiraia aliapa kwa mshangao Jumatatu kutoa nafasi kwa makundi ya kiraia kuunda serikali mpya ya mpito.

Lakini muungano mkuu wa kiraia The Forces for Freedom Change (FFC) ulitoa wito wa kuendeleza shinikizo la umma mitaani na kutupilia mbali hatua ya Burhan na kusema ni mbinu ya ujanja wa uwazi. Hotuba ya kiongozi wa mapinduzi ni hila kubwa na mbaya zaidi kuliko mapinduzi ya Oktoa 25 kiongozi wa FFC, Taha Othman alisema.

Mgogoro huo utaisha kwa viongozi wa mapinduzi kujiuzulu na vikosi vya mapinduzi kuunda serikali ya kiraia. Maandamano pia yalienea katika miji mingine Jumanne ikiwa ni pamoja na Wad Madani uliopo kilomita 200 kusini mwa mji mkuu ambapo mamia ya waandamanaji walifanya maandamano ya kukaa chini kulingana na mashahidi.