Democratic na Republican hawajakubaliana jinsi ya kuzuia umiliki bunduki holela Marekani

Mfano wa duka linalouza silaha Marekani

Maseneta wa Democtaric na Republican hawajakubaliana Alhamis kuhusu jinsi ya kuzuia bunduki kutoka kwa watu hatari huku wadau wakijitahidi kukamilisha maelezo ya maafikiano ya ghasia za bunduki kwa wakati na muda wao waliojiwekea kupiga kura katika bunge wiki ijayo.

Wabunge walisema bado wamegawanyika kuhusu jinsi ya kufafanua wapenzi wanyanyasaji ili waweze kuzuiliwa kisheria kununua bunduki. Kutokukubaliana huko hakujapatiwa ufumbuzi juu ya mapendekezo ya kupeleka pesa kwenye majimbo yenye sheria zilizowekewa angalizo jekundu ambayo yanaruhusu mamlaka kwa muda kuwanyang’anya bunduki wamiliki wa bunduki iwapo wanaonekana na mahakama kuwa ni hatari na kwa majimbo mengine kwa kufuata program zao za kuzuia ghasia.

Seneta John Cornyn wa jimbo la Texas anayeongoza mashauriano kwa upande wa Republican alionekana kutofurahishwa wakati alipoondoka Alhamis kwenye kikao cha faragha kilichochukua takribani saa mbili akisema alikuwa anasafiri kurudi nyumbani kwake.

Mashauriano hayo katika mwaka wa uchaguzi yalichochewa na ufyatuaji risasi wa mwezi uliopita kwenye duka la vyakula katika mji wa Buffalo kwenye jimbo la New York na shule ya msingi ya Robb kwenye mji wa Uvalde katika jimbo la Texas ambapo jumla ya watu 31 waliuawa kwenye matukio hayo.