Rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, amemteua mbunge kutoka baraza kuu la bunge Hamza Abdi Barre kuwa Waziri Mkuu mpya.
Mohamud alitoa tangazo hilo kwenye makazi ya Rais siku ya Jumatano. “Nimezingatia uamuzi wangu baada ya kutathmini ufahamu, uzoefu, pamoja na uwezo wa Hamza, kisha nikafikia hitimisho kwamba yeye ndio mtu sahihi, ambaye anaweza kutekeleza jukumu hili jipya katika Somalia hii mpya kwa wakati huu mpya” alisema.
Aliwataka wabunge kumwidhinisha Waziri Mkuu mpya haraka na kusema amemtaka Barre kuendeleza vipaumbele muhimu vya serikali mpya ikiwa ni pamoja na usalama, kukabiliana na ukame, maridhiano, maendeleo ya jamii na kukabiliana na majanga ya hali ya hewa.