Vikosi vya Russia vilishambulia kwa mabomu kiwanda cha kemikali kinachohifadhi mamia ya wanajeshi na raia katika mji wa Sievierodonetsk huko mashariki mwa Ukraine siku ya Jumapili lakini gavana wa mkoa wa Luhansk alisema kiwanda hicho kiko chini ya udhibiti wa Ukraine.
Gavana Serhii Haidai alisema huo ni uongo unaotolewa na wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Russia kwamba wanajeshi 300 hadi 400 wa Ukraine wamekwama katika kiwanda cha Azot pamoja na mamia ya raia.
Eneo la kiwanda hicho linapigwa risasi Haidai alisema. Mapigano yanaendelea kwenye viunga vya jiji katika mitaa karibu na kiwanda hicho. Alisema moto mkubwa ulizuka kwenye kiwanda siku ya Jumamosi wakati wa shambulizi la Russia.
Russia inadai kwamba tayari inadhibiti asilimia 97 ya mkoa wa Luhansk. Lakini kuuteka mji wa viwanda wa Sievierodonetsk wenye wakaazi laki moja kabla ya vita bado ni muhimu kwa lengo pana la Moscow kudhibiti eneo la mashariki la Donbas ambalo linajumuisha mikoa ya Luhansk na Donetsk.