Finland imetangaza rasmi kuomba uanachama wa NATO

Rais wa Finland Sauli Niisto (R) akiwa na Waziri Mkuu wake Sanna Marin ambapo rais anatangaza rasmi nia ya kuomba uanachama kwa NATO akiwa Helsinki, May 15, 2022.

Finland ilitangaza rasmi Jumapili kwamba inakusudia kuomba uanachama katika muungano wa kijeshi wa magharibi wa NATO ikipuuza onyo la Rais wa Russia Vladmir Putin kwamba hatua hiyo itaathiri vibaya uhusiano wa amani kati ya nchi hizo jirani.

Rais Sauli Niinisto na Waziri Mkuu Sanna Marin walitangaza azma ya uanachama wa NATO katika Ikulu ya Rais huko Helsinki. Hii ni siku ya kihistoria Niinisto alisema. Enzi mpya inaanza.

Tangazo la Finland kwamba inataka kuingia katika muungano wa kijeshi unaotawaliwa na Marekani wenye wanachama 30 ulioundwa baada ya vita vya pili vya dunia ulitarajiwa kufuatia uvamizi wa Russia nchini Ukraine hapo Februari 24 ambapo mashambulizi bado yanaendelea. Jirani na Finland upande wa magharibi Sweden pia inatarajiwa kutaka kuingia katika muungano huo na kumaliza karne mbili za kutojiunga na ushirika huo. Chama kinachotawala nchini Sweden siku ya Jumapili kiliondoa upinzani wake wa kujiunga na NATO.