Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alipimwa Jumatano na alikutwa na maambukizi ya COVID-19 na atafanya kazi kwa njia ya mtandao, wizara ya mambo ya nje ilisema.
Waziri amepata chanjo kamili pamoja na Booster dhidi ya virusi na anazo dalili ndogo tu, wizara hiyo ilisema katika taarifa. Blinken hajamuona Rais Joe Biden ana kwa ana kwa siku kadhaa na hivyo Biden hachukuliwi mtu wa karibu katika suala hili, taarifa ilisema.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Ned Price alisema kuwa Blinken hatoweza kutoa tena hotuba iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu kuhusu sera ya China ambayo ilipangwa Alhamis. Anatarajia kurejea kwenye jengo la wizara hiyo na kuanza tena ratiba yake kamili pamoja na safari haraka iwezekanavyo ilisema taarifa hiyo.
Blinken alikuwa miongoni mwa wageni waliojazana katika hoteli ya Washington siku ya Jumamosi kwa ajili ya chakula cha jioni cha kila mwaka cha chama cha waandishi wa habari wa White House. Trevor Noah mchekeshaji ambaye alimtambulisha Rais Biden alitania kuhusu chakula hicho cha jioni kuwa ni tukio kubwa la kusambaza virusi.