WHO inapendekeza ongezeko la matumizi ya chanjo ya kwanza ya Malaria Afrika

Mfano wa mbu anayesababisha ugonjwa wa Malaria ambao unauwa watu wengi duniani

Jumatatu April 25 ni siku ya Malaria Duniani, shirika la afya Duniani (WHO) linapendekeza upanuzi wa matumizi ya chanjo ya kwanza ya malaria na kuitaja kuwa inawezekana kuleta mabadiliko katika vita dhidi ya Malaria.

Malaria ni ugonjwa unaozuilika, na unaotibika. Hata hivyo kila mwaka malaria huwakumba zaidi ya watu milioni 200 na kuua zaidi ya laki sita. Vifo vingi kati ya hivi karibu nusu milioni, miongoni mwao ni watoto wadogo huko barani Afrika. Hivyo basi ina maana kila sekunde 60 mtoto hufariki kwa malaria.

Licha ya habari hizi mbaya, mtazamo wa kudhibiti malaria unatia matumaini kutokana na kutengenezwa kwa chanjo ya kwanza ya malaria Duniani. Shirika la afya duniani linayaita mafanikio haya ya kihistoria kwa sayansi.

Mpango wa majaribio ulianzishwa mwaka 2019 nchini Ghana, Kenya na Malawi.Tangu wakati huo, shirika la afya duniani linaripoti zaidi ya watoto milioni moja katika nchi hizo tatu wamepokea chanjo ya malaria.

Mary Hamel, ni mkuu wa mpango wa utekelezaji wa chanjo ya malaria katika WHO. Anasema mpango wa majaribio wa miaka miwili umeonyesha chanjo hiyo ni salama, inawezekana kutoa na kupunguza ugonjwa hatari wa malaria.

“Tuliona kupungua kwa asilimia 30 kwa watoto wanaoletwa hospitali na ugonjwa mbaya wa Malaria. Pia tuliona kupungua kwa karibu asilimia kumi kwa vifo vyote vya watoto vinavyosababishwa na malaria. Kama chanjo hiyo itasambazwa kwa wingi, inakadiriwa kwamba inaweza kuokoa maisha ya watoto wengine 40 hadi 80,000 kila mwaka”.

WHO inaripoti GAVI, Ushirika wa chanjo utatoa zaidi ya dola milioni 155 kusaidia kupanua uzinduzi wa chanjo ya malaria kwa nchi zinazostahiki GAVI, huko Afrika, kusini mwa jangwa la sahara.

Chanjo dhidi ya malaria ilikuwa ikitengenezwa kabla ya chanjo ya COVID-19 kutengenezwa. Hamel anasema WHO imejifunza mengi kutokana na juhudi hizo ambazo zinaweza kutumika katika utengenezaji wa chanjo za malaria siku zijazo.

“Tunajua kumekuwa na mifumo mipya iliyojitokeza tangu chanjo ya COVID ikijumuisha jukwaa la mRNA na hivi sasa watengenezaji wa mojawapo ya chanjo ya mRNA wanatazamia kutengeneza chanjo ya malaria kwa kutumia jukwaa hilohilo”.

Julai mwaka 2021 BioNTech, mtengenezaji wa chanjo ya Pfizer-BioNTech COVID-19 ilitangaza inataka kuendeleaz mafanikio hayo kwa kutengeneza chanjo ya malaria kwa kutumia teknolojia ya mRNA. Kampuni hiyo ya kutengeneza dawa inasema inalenga kuanza majaribio ya kimatibabu kufikia mwisho wa mwaka huu.