Marekani inafuatilia mauaji ya zaidi ya watu 200 nchini Mali

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Marekani, Ned Price. March 10, 2022.

Marekani inafuatilia kwa karibu taarifa mbaya za idadi kubwa ya watu waliouawa katika kijiji kimoja huko kati-kati mwa Mali msemaji wa wizara ya mambo ya nje Marekani, Ned Price alisema Jumapili.

Jeshi la Mali lilisema Jumamosi kwamba limewaua zaidi ya wanamgambo 200 wa kiislam katika mapigano ya karibuni katika muda wa mwezi mmoja wa ghasia zinazozidi kusambaa. Mivutano na nchi za magharibi imeongezeka tangu hatua iliyochukuliwa na utawala wa kijeshi wa Mali kuchelewesha uchaguzi wa kidemokrasia mwezi Februari pamoja na ushirikiano wake na wakandarasi wa kijeshi binafsi wa kundi la Wagner kutoka Russia.

Katika taarifa yake Price alisema kulikuwa na ripoti zinazokinzana kuhusu ni nani aliyehusika na mauaji hayo yaliyotokea mwishoni mwa mwezi machi katika kijiji cha Moura, kiasi cha kilometa 400 kaskazini-mashariki mwa mji mkuu Bamako.