Rais Kiir na mpinzani wake Machar wafikia makubaliano ya kuleta amani Sudan Kusini

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir (L) na kiongozi wa upinzani Riek Machar, katika mazungumzo yao ya kurejesha amani mjini Juba, Sudan Kusini, Dec. 17, 2019.

Katika kile ambacho kimepongezwa ni mafanikio makubwa viongozi hasimu wa Sudan Kusini walikamilisha makubaliano Jumapili, kuhusu kipengele muhimu cha kijeshi katika mkataba wa amani uliokwama na kuapa kunyamazisha bunduki zao.

Rais Salva Kiir na hasimu wake Makamu Rais Riek Machar walikubaliana juu ya kuundwa kwa komandi ya pamoja ya kijeshi mojawapo ya masuala kadhaa ambayo yamekwama katika utekelezaji wa mkataba wa mwaka 2018 wa kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano vya umwagaji damu nchini humo.

Mivutano kati ya vikosi vinavyomtii Kiir na kiongozi wa zamani wa waasi Machar, iliongezeka hivi karibuni na kuzua khofu ya kurejea kwenye mzozo kamili katika taifa hilo changa zaidi duanini. Amani ni kuhusu usalama na leo tumefikia hatua muhimu alisema Martin Abucha ambaye alitia saini makubaliano hayo kwa niaba ya chama cha upinzani cha SPLM/A-IO. Bunduki lazima ziwekwe chini.

Waziri katika ofisi ya rais Barnaba Marial Benjamin, alipongeza makubaliano hayo, yaliyofikiwa kufuatia upatanishi wa nchi jirani ya Sudan kama hatua ya muhimu ambayo inafungua njia kwa serikali thabiti ya Jamhuri ya Sudan Kusini.