Jaji Ketanji ahojiwa na seneti kwa siku ya pili

Jaji Ketanji Brown Jackson akijibu maswali mbele ya kamati ya seneti mjini Washington, March 22, 2022.

Katika siku ya pili ya vikao vya seneti kuhusu uteuzi wake katika mahakama ya juu, jaji Ketanji Brown Jackson, alikabiliwa na maswali kwa saa kadhaa kutoka kwa wanachama wa kamati ya sheria ikizingatia kila kitu kuanzia falsafa yake ya mahakama kwa ujumla hadi maswali mahususi kuhusu maamuzi ambayo aliyatoa.

Jackson, mwanamke wa kwanza mweusi kuteuliwa katika kiti cha mahakama ya juu zaidi ya taifa, alifikia utaratibu wa kuulizwa maswali baada ya siku moja wanachama wa kamati ya sheria kutumia saa kadhaa kutoa taarifa zao ufunguzi. Wanachama wa Republican kwenye jopo hilo walikuwa wameashiria kwamba wangempinga katika masuala mbali-mbali. Siku ya jumanne kila mwanachama alikuwa na dakika 30 za kumhoji Jackson.

Wa-Democrat walitumia muda wao mwingi waliopewa kuzungumza kwa ukaribu na Jackson, badala ya kuuliza maswali ya moja kwa moja. Walipishana na wa-Republican ambao kwa ujumla walimshinikiza Jackson, juu ya mada kuanzia ndoa za watu wa jinsia moja hadi kuwahukumu waliopatikana na hatia ya kuwa na picha za ngono za watoto.