Taliban kwa mara nyingine imeiomba Marekani kutoa mabilioni ya dola iliyozuia baada ya mazungumzo ya siku mbili mjini Doha, wakati Afghanistan ambayo inategemea sana misaada ya kimataifa inaendelea kukumbwa na mzozo wa kiuchumi.
Wajumbe wa Afghanistan wameomba pia nchi yao iondolewe kwenye orodha ya nchi zinazohatarisha usalama na iondolowe vikwazo katika mikutano iliyoongozwa na waziri wa mambo ya nje wa Taliban Amir Khan Muttaqi na Tom West, mjumbe maalumu wa Marekani kwa ajili ya Afghanistan.
Ilikuwa duru ya pili ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili ambayo yalifanyika nchini Qatar tangu Marekani kumaliza vita vya miaka 20 nchini Afghanistan na Taliban kuchukuwa tena madaraka.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Afghanistan Abdul Qahar Balkhi aliandika kwenye Twitter kwamba ‘waakilishi wa pande mbili walijadili masuala ya siasa, uchumi, afya na elimu, vile vile kuipatishia Afghanistan pesa za benki na pesa taslimu’.
Washington imezuia karibu dola bilioni 9 na nusu kama mali za benki kuu ya Afghanistan. Shirika la kimataifa la fedha(IMF) na benki kuu ya dunia zilizitisha pia shughuli zao nchini Afghanistan, kwa kuzuia msaada pamoja na dola milioni 300 na 40 katika pesa za akiba zilizotolewa na IMF mwezi Agosti.