Tshisekedi aahidi kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa wa Kongo

Rais Felix Tshisekesdi akiwasili Windhoek Namibia Februari 26 2019. (Facebook/Fatshi News)

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameahidi kuwaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa na kupanga kuwarudisha wale wote walokimbia n’gambo kutokana na sababu za kisiasa.

Akizungumza katika sherehe za kuzindua malengo yake ya kisiasa, usalama na uchumi mnamo siku 100 za kwanza za utawala wake kwenye uwanja wa Mabadilishano ya Mawazo, mtaa wa Limete, mjini Kinshasa siku ya Jumamosi, rais Thisekedi alisema atahakikisha wizara ya sharia na mfumo wa mahakama zinaendeshwa na watu waaminifu na wenye maadili yasiyo na dosari.

“Mnamo siku kumi zijazo nitatoa msamaha wa rais kuachiliwa huru wafungwa walohukumiwa na mahakama. Na katika kuimarisha utaratibu wa kidemokrasia nchini mwangu , nimeamua kwamba lengo langu kuu mnamo siku 100 za kwanza kupunguza mvutano wa kisiasa.” alisema rais Tshisekedi

Alisema atamamrisha waziri wa sharia kuwaachilia huru wale wote walokamatwa kwa sababu za kueleza maoni yao, hasa wakati wa mikujtano ya kisiasa kabla ya uchaguzi waDisemba 30.

Kuhusiana na utawala bora kiongozi huyo aliyechukua madaraka Januari 24, ameahidi kutayarisha kanuni za maadili ya vyombo vya serikali na kusimamia utekelezaji wake.

Tshisekedi alitowa pia ahadi ya kufanya marekebisho makubwa katika mazingira ya biashara kwa kutowa kanuni mpya za uchimbaji madini na kuhakikisha kuna mikataba ambayo pande zote husika zinanufaika kwa usawa.

Ili malengo yake yaweze kufanikiwa kiongozi huyo aliyechukua madaraka kuytoka Joseph Kabila amesema ana hitaji ushirikiano na Wakongo wote kwa kubadli maadili na mawazo yao kwa kuheshimu haki za binadamu, haki za kiraia, na uhuru wa kila aina kwa kila mtu.