Rais Macron kulihutubia taifa kujaribu kumaliza maandamano

Waandamanaji walova koti manjano wasimama karibu na mti unaowaka moto karibu na mnara Arc de Triomphe mtaa wa Champs-Elysees

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, anatazamiwa kukutana na wakuu wa vyama vya wafanyakazi, wakuu wa makampuni, na asasi za kiraia, mjini Paris, Jumatatu asubuhi kabla ya kulihutubia taifa katika juhudi za kumaliza malalamiko na maandamano yanayongozwa na vuguvugu la watu wanaova makoti manjano.

Uwamuzi huo umechukuliwa kufuatia maandamano mengine makubwa katika mji mkuu wa Paris siku ya Jumamosi ambao ulosababisha hasara kubwa ya mali, ingawa haukuwa na ghasia kama Jumamosi wiki iliyopita.

Polisi wa Ufaransa watumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji mjini Paris.

Wizara ya mambo ya ndani inaeleza kwamba karibu watu 1 700 walikamatwa baada ya karibu watu 350 000 kujitokeza kutoka kila pembe ya nchi na kuandamana katika mitaa ya Paris.

Katika ujumbe wa tweeter Rais Macron aliwasifu maafisa wa usalama kwa kuweza kudhibiti maandamano hayo.

Ofisi ya meya wa jiji la Paris inaeleza kwamba polisi waliweza kudhibiti vyema maandamano hayo kulingana na maandamano ya wiki iliyopita, lakini kueleza kwamba uharibifu ulikuwa mkubwa zaidi.

Maandamano hayo yaliyoanza kwa malalamiko dhidi ya kongezwa kodi ya mafuta ya dizeli, yaliyongozwa na madereva wa magari, yamegeuka kua vuguvugu la kupinga ughali wa maisha na kumtaka rais Macron kujiuzulu wakidai kwamba sera za kiongozi huyo aliyekua afisa wa benki zinalinda maslahi ya matajiri dhidi ya wananchi.