Rais Buhari kuwapokea wasichana 82 wa Chibok waloachiwa huru

Wasichana wa Chibok waloachiliwa waelekea ndani ya helikopta Mei 6, 2017

Femi Adesina, mshauri maalum wa rais Muhammadu Buhari, amewaambia waandishi habari kwamba wasichana waloachiliwa huru wamewasili katika mji mkuu wa Abuija na walipokelewa na mkuu wa utawala Alhaji Abba Kyari.

Taarifa ya ofisi ya rais iliyotolewa Jumamosi jioni, imeshukuru Chama cha Kimataifa cha Msalaba Mwekundu na serikali ya Uswisi kwa kusaidia kupatikana kwa wasichana hao baada ya majadiliano marefu na wanamgambo wa Boko Haram.

Magari ya Msalaba Mwekundu yawasafirisha wasichana wa Chibok waloachiwa huru

Taarifa hiyo inaeleza kwamba, "baada ya majadiliano marefu, idara zetu za usalama zimeweza kuwarudisha wasichana wetu, katika mpango wa kubadilishana wafungwa na baadhi ya watuhumiwa wa Boko Haram walokua wanashikiliwa na idara za usalama."

Hakuna habari zaidi zilizotolewa kiuhusu idadi ya watuhumiwa waloachiliwa wala kutajwa ni nani.

Wasichana hao walowasili Nigeria Jumamosi karibu miezi sita baada ya kuachiliwa wenzao 21 waloachiliwa huru kutokana na msaada wa wapatanishbi wa kimataifa walionekana wachofu na walokonda.

Wasichana 276 wa shule ya Chibok kaskazini ya Nigeria walitekwa nyara 2014, wakiwa ni miongoni mwa mamia ya wanigeria walotekwa na kundi hilo lenye kufuata itikadi kali za kislamu mnamo miaka minane ya uwasi wake kaskazini mwa Nigeria.