Azali atangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais Comoros

Rais wa zamani wa Comoros Azali Assoumani

Kiongozi wa upinzani Kanali Azali Assoumani ametangazwa kua mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais ulofanyika tarehe 10 April 2016.

Mahakama ya Katiba ya Comoros ilitangaza Jumapili kwamba, imethibitisha matokeo ya marudio katika wilaya 13 za kisiwa cha Nzwani, cha pili kwa ukubwa na hivyo kumpatia ushindi Assoumani kama ilivyotangazwa na tume ya uchaguzi, CENI.

Matokeo hayo yamewafurahisha Wakomoro walokua na wasi wasi kwamba serikali huwenda inajaribu kubadili matokeo ya uchaguzi ili kumpatia ushindi mgombea wake Mohamed Ali Soilihi, jambo ambalo lingeliweza kuzusha ghasia katika visiwa hivyo vya bahari ya Hindi kulingana na wachambuzi wengi.

Assoumani aliyepata asili mia 41.43 za kura katika uchaguzi ulokua na ushindani mkubwa, ni kiongozi wa 8 kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia visiwani humo na aliwahi kua rais kati ya 1999 hadi 2006.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma wamepongeza Wacomoro kwa kushiriki kwa amani na utulivu katika uchaguzi wa rais na majimbo.