Mtoto Anusurika Ajali ya Ndege, Sudan Kusini

Ramani ya Sudan Kusini ikionyesha pale mji wa Juba ulipo.

Maafisa wanasema mtoto mmoja amenusurika katika ajali ya ndege iliyotokea punde baada ya kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Juba, Sudani Kusini.

Kwa mujibu wa taarifa, ajali hiyo ya ndege ya mizigo aina ya Antonov imesababisha vifo vya watu 32.

Ndege hiyo iliyotengenezwa Russia, ilianguka mita 800 kutoka barabara ya kurukia ndege Jumatano, na kuangukia kwenye msitu uliopo pembezoni mwa mto Nile Mweupe.

Bado haijafahamika kama wale wote walioathirika walikuwa arthini ama walikuwemo kwenye ndege hiyo wakati wa ajali.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba ndege hiyo ilikuwa na jumla ya watu 18 ikijumuisha wafanyakazi sita wa ndege.

Kwa mujibu wa taarifa wafanyakazi wa ndege hiyo walijumuisha Wamarekani watano na raia mmoja wa Russia na wote walipoteza maisha.

Taarifa zaidi zinasema ndege hiyo ilikuwa ikielekea katika viwanja vya mafuta katika jimbo la Upper Nile.