Wakenya wapata ushindi wa kihistoria Beijing

Asbel Kiprop wa Kenya akinyakua ushindi katika mbiyo za mita 1500, huko Beijing 2015

Wakenya washerehekea ushindi wa kihistoria katika michezo ya Dunia ya Riadha, IAAF, yaliyomalizika hujo Bejing, China siku ya Jumapili, kwa kuongoza katika orodha ya medali jumla.

Asbel Kiprop alimaliza kwa ustadi mkubwa mbiyo za mita 1 500, na kushangiriwa na watazamaji elfu 80 wa uwanja wa kisasa wa Bird’s Nest huko Bejing, alipomaliza baada ya kuwa nyuma katika rauni ya mwisho, akiwashinda wenzake wote katika mita ya 20 za mwisho. Kiprop alimaliza mbiyo za mita 1500 kwa kutumia muda wa dakika 3 sekunde 34.40, akifuatwa na Mkenya mwenzake Elijah Motonei Manangoi.

Mkenya Eunice Jepkoech Sum, akisherehekea ushindi wake wa nafasi ya tatu katika mbiyo za mita 800

Kabla ya ushindi wa Kiprop, Helah Kiprop alijinyakulia medali ya fedha katika mbiyo za marathon wanawake na hivyo kuipatia Kenya jumla ya medali 16, saba za dhahabu, sita za fedha na tatu za shaba

Marekani ambayo daima imekuwa ikichukua nafasi ya kwanza imeondoka na medali nyingi zaidi, 18 kwa ujumla lakini imechukua nafasi ya tatu kwa kuondoka na medali sita za dhahabu, sita za fedha na sita za shaba.

Jamaica nayo imeweka pia historia yake kwa kuchukua nafasi ya pili ikiondoka na medali 12, ikiwa na medali saba za dhahabu mbili za fedha na tatu za shaba.

Wakenya wanaripotiwa kusherehkea kote nchini Jumapili kwa ushindi huo wa kihistoria, kwani mara ya mwisho Kenya kuwika namna hii ilikua 2011 huko Korea ya Kusini iliponyakua medali 17 na kuchukua nafasi ya 3 kwa ujumla nyuma ya Marekani na Rashia.

Score table