Rais wa Misri asaini sheria kali dhidi ya ugaidi.

Rais wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi akizungumza na wananchi kwenye msiba wa mwendesha mashitaka mkuu wa Misri Hisham Barakat, akiwa na wanafamilia wake.

Rais wa Misri Abdelk Fatah El Sisi amesaini sheria mpya ya kupambana na ugaidi jana Jumapili ambayo inatoa hukumu ya kifo na kifungo cha maisha jela kwa baadhi ya makosa na pia kutishia faini kubwa kwa ripoti za uongo juu ya mashambulizi ya kigaidi.

Bw.Sisi aliahidi mwezi Juni kuweka sheria kali za kupambana na ugaidi baada ya mwendesha mashitaka mkuu wa Misri kuuwawa kwa bomu . Makundi mawili ya wanamgambo yalidai kuhusika na shambulizi. Lakini rais huyo amelishutumu kundi la Muslim Brotherhood ambalo serikali yake imelitaja ni taasisi ya kigaidi na kulikandamiza tangu alipoongoza kuondolewa mamlakani kwa rais mwenye msimamo wa serikali ya kiislam Mohamed Morsi Julai 2013.

Chini ya sheria mpya wale wanaoongoza au kuanzisha makundi ya kigaidi huenda wakakabiliwa na adhabu ya kifo. Kufadhili ugaidi kunaweza kupelekea adhabu ya kifungo cha maisha wakati kuchochea kitendo cha kigaidi au kujiandaa kuchochea shambulizi kunapelekea kifungo jela.