Mataifa makuu ya dunia yamefikia makubaliano ya kihistoria na Iran juu ya mpango wa nuklia wa Teheran mjini Vienna Austria. Mkataba huo utapunguza uwezo wa Iran kutengeneza silaha za nuklia ili nayo iweze kuondolewa kwa awamu vikwazo vya kiuchumi.
Mkuu wa masuala ya kigeni wa Jumuia ya Ulaya Federica Mogherini na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Javad Zarif walitangaza mkataba huo mjini Vienna kufuatia wiki kadhaa ya mazungumzo marefu juu ya kukamilisha kila kipengele cha mkataba huo.
Rais Barack Obama akizungumza mara baada ya kutangazwa mkataba huo amesema"mkataba huu unadhihirisha kwamba diplomasia ya Marekani inaweza kupelekea kupatikana mabadiliko ya kwerli na ya maana."
Rais alisema atatumia kura yake ya turufu kupinga sheria yeyote katika bunge la Marekani ambayo itajaribu kuzuia mkataba huo. "Mkataba unatowa fursa ya kusonga mbele kwa njia mpya." aliongeza kusema Obama.
Kwa mara ya kwanza katika kitendo cha Nadra hotuba ya kiongozi wa Marekani ilitangazwa moja kwa moja na vituo vyote vya televisheni nchini Iran.
Na mara baada ya hotuba ya Obama hapa Washington, Rais wa Iran Hassan Rouhani alipongeza makubaliano hayo na kusema "ukurasa mpya" umeanza katika uhusiano na dunia.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry, akizungumza mjini Vienna Jumanne, alikaribisha mkataba lakini alionya kwamba "ikiwa Iran itashindwa kwa njia yeyote kuheshimu' ahadi zake basi vikwazo vitarudishwa mara moja.
Your browser doesn’t support HTML5