Umoja wa Mataifa waipinga Sudan Kusini

Umoja wa mataifa unasema Sudan Kusini imeamua kumfukuza naibu muwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ameshutumu hatua hiyo na kuitaka Sudan Kusini, kubadili maamuzi hayo haraka.

Umoja huo umesema jana Jumatatu kwamba Sudan Kusini, inataka kumuondoa Toby Lanzer, raia wa Uingereza ambaye ni mratibu wa masuala ya kibinadamu kwa Sudan.

Msemaji wa bwana Moon, amesema, bwana Lanzer, alikuwa kiungo katika kushughulikia mahitaji ya kibinadamu ya mgogoro unaoathiri jumuiya kadhaa nchini humo, na kuhakikisha misaada hiyo inawafikia wale walio katika mahitaji.