Waziri wa wizara ya Usalama wa ndani Marekani Jeh Johnson anasema serikali inachukulia kwa uzito mkubwa vitisho vilivyotolewa na wanamgambo wa Somalia vya kushambulia maeneo yenye maduka makubwa katika nchi za Magharibi.
Waziri Johnson alizungumza na waandishi habari Jumapili mara baada ya ukanda wa video kutolewa na wanamgambo wa al-Shabab kutoka Somalia, ukielezea kuwa watashambulia maeneo yenye maduka makubwa.
Johnson alisema vitisho vya kigaidi dhidi ya dunia vimeibuka kutokana na makundi ya wanamgambo yanayotoa mwito kwa watu binafsi kufanya mashambulizi ya kigaidi ndani ya nchi zao. Alisema “tumepita kipindi ambacho makundi kama haya yalikuwa yanatuma washambuliaji wao katika nchi za kigeni baada ya kupewa mafunzo kwingineko.”
Kundi la al-Shabab lilikiri kutekeleza shambulizi la kigaidi katika maduka ya kifahari ya Westgate jijini Nairobi,Kenya Septemba mwaka 2013, ambapo watu 67 waliuawa.
Katika ukanda huo wa video, magaidi wa al-Shabab wamesema watashambulia eneo la maduka liitwalo Mall of Amerika katika jimbo la Minnesota nchini Marekani na maeneo mengine ya Canada na Uingereza.