Mamilioni ya watu wanaoishi maeneo ya mashariki mwa Marekani wanaendelea kukabiliana na hali ngumu ambayo imetokana na kimbunga cha theluji ambacho kimesababisha kusitishwa kwa usafiri wa ndege na misongamano ya magari.
Awali watabiri wa hali ya hewa walisema kwamba theluji ingeanguka kwa zaidi ya kiwango cha mita moja ikiandamana na upepo mkali mapema Jumanne . Lakini hali hiyo haionekani kuwa mbaya kama ilivyotarajiwa. Wamesema eneo la New England ndilo limeathiriwa zaidi.
Idara ya kitaifa ya hali hewa iliripoti takriban sentimita 15 jijini New York huku theluji zaidi ikitarajiwa kuanguka jijini humo. Katika upande wa kaskazini maeneo ya Boston, Providence na Rhode Island yanatarajiwa kupata sentimita 50 hadi 60 za theluji.
Wakazi wa Boston na New York waliozungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika-VOA walisema hakuna huduma zozote za usafiri, si wa ndege au barabara. Wengi walinunua vyakula, maji na bidhaa nyingine za kimsingi kwa sababu huenda wakabaki majumbani kwa siku tatu.