Burkina Faso wapata Rais wa muda

Luteni Kanali Yacouba Isaac Zida aliyekabidhi madaraka kwa waziri wa zamani wa mambo ya nje,Burkina Faso, kuwa Rais.

Maafisa nchini Burkina Faso wamemteuwa waziri wa zamani wa mambo ya nje Michel Kafando kuwa rais wa muda mwenye jukumu la kuongoza kurejesha utawala wa kiraia.

Kamati iliyoundwa na wanasiasa, wawakilishi wa jeshi, viongozi wa kiraia, na kidini ilitangaza uchaguzi wa bwana Kafando jumatatu, siku moja baada ya kuanza mazungumzo ya kujaza wadhifa huo.

Kiongozi wa upinzani Zephirin Diabre alielezea chaguo hilo ni muafaka. Bwana kafando, atamteuwa waziri mkuu atakayeunda serikali ya muda.

Akiwahutubia waandishi wa habari jumatatu, Rais huyo mpya alisema serikali yake itafanya kadri iwezavyo kuleta mafanikio katika kipindi cha mpito.

Jeshi la Burkina Faso lilichukua madaraka mwezi uliopita baada ya mtawala wa muda mrefu wa Blaise Compaore aliyejiuzulu kufuatia maandamano dhidi ya juhudi zake za kubadilisha katiba ili agombee tena urais mwakani.