Raila:Uhuru usiwanyamazishe magavana

Raila Odinga kiongozi wa ODM akihutubia umati wa watu kwenye uwanja wa Uhuru Park Nairobi, July 7, 2014.

Kiongozi wa mungano wa upinzani wa Cord, Raila Odinga ameituhumu serikali inayoongozwa na mungano wa Jubilee huko Kenya kwa kujaribu kuwanyamazisha magavana wanaounga mkono juhudi za kuitisha kura ya maoni juu ya katiba.

Katika matukio ambayo yalionekana kama Kenya inarudi katika kampeni za uchaguzi, Rais Uhuru Kenyatta alitoa wito Jumapili kwa magavana wa mungano wake wanaounga mkono mabadiliko ya katiba kujiuzulu na kupigania upya madaraka chini ya mungano mwengine.

Akizungumza mjini Kericho Rais Kenyatta alisema magavana wanachukua hatua dhidi ya matakwa ya ajenda ya maendeleo ya muungano wa Jubilee, na kwamba mungano wao umeungana kupinga jaribio lolote la kuitisha kura ya maoni.

Akizungumza huko Kibera hiyo hiyo Jumapili, Bw. Odinga alisema, "hebu nimjibu, ni lini mungano wa Jubilee ulikutana na kupitisha azimio la kupinga kura ya maoni? Amepata wapi uwamuzi huo?"

Alkizungumza na Sauti ya Amerika, mwenyekiti wa magavana wa Kenya, gavana wa County ya Bomet, Isaac Ruto, anasema hawatotishika na siasa ya vitisho ambavyo vinaweza kuleta mvutano zaidi nchini.

Bw. Ruto, ambae ni mwanachama wa Jubilee ametuhumiwa na rais kwa kuisaliti serikali ya Jubilee.