Jaji Leon asema kukusanya mawasiliano ya simu ni kukiuka katiba ya Marekani

Waandamanaji wakipinga kitendo cha NSA nje ya bunge la Marekani wakilitaka bunge kuchunguza hatua hiyo.

Jaji mmoja wa Marekani anasema kitendo cha serikali ya Marekani kukusanya kwa siri rekodi za simu za mamilioni ya wamarekani huwenda kikawa ni kitendo kinacho kiuka katiba.

Katika juhudi za kuzuia shambulizi jingine la kigaidi kwenye ardhi ya Marekani , idara ya usiri ya usalama wa taifa imekuwa kwa miaka kadhaa ikikusanya idadi kubwa ya namba za simu ambazo watu wamepiga pamoja na kuweka tarehe na muda wa mazungumzo hayo, ingawa hawasikilizi kinachozungumzwa.

Lakini jana Jaji Richard Leon hapa Wahington alisema hawezi kufikiri njia nyingine ile ya kuingilia kiholela bila kubagua katika maisha ya watu binafsi kama vile serikali kukusanya taarifa hizo bila ruhusa ya mahakama.

Katika uwamuzi wa mahakama kupinga uchunguzi huo , Leon amesema upelelezi huo unakiuka kifungu cha katiba ya Marekani kinazuia upekuzi kwa watu bila kibali.