Zoezi la kuhesabu kura laendelea Kenya.

Wakenya wakisubiri kupiga kura katika shule ya msingi ya Westland, Nairobi .


Mombasa ni baadhi ya maeneo yaliyochelewesha matokeo ya kura katika uchaguzi mkuu nchini Kenya zilizopigwa Jumatatu huku vituo maalum vya kutangazia matokeo vikiyasubiri kwa muda mrefu kutoka vituo vya mashinani.

Sababu kubwa iliyotajwa ni matatizo ya vifaa au mitambo iliyogharimu serikali mamilioni ya pesa ilijulikanayo kama mashine za BVR.

Tatizo lingine ni mashambulizi kati ya Jumapili usiku na mapema jumatatu, ambapo zaidi ya watu 10 waliuawa wakiwepo maafisa waandamizi wa polisi wa wilaya ya Changamwe, Mombasa.

Kituo kikuu cha kutangaza matokeo yote kutoka kaunti ya Mombasa, kipo katika Bandari, na afisa wa timu ya uchaguzi anayesimamia hapo Laban Mwashighadi anasema vituo vingine katika jimbo la Kilifi vilifungwa mapema jumatatu baada ya maafisa waliosimamia zoezi hilo, kupokea vitisho kutoka kwa watu waliopanga kuwavamia.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka Kenya –Issack Hassan amethibitisha kuhusu hilo.

Wakati huo huo watu kadhaa wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa vuguvugu la Mombasa Republican –MRC wameshtakiwa kuhusiana na mauaji ya maafisa wanne wa polisi, waliokuwa wanafanya doria kabla ya uchaguzi huo kuanza.

Majina yao yamesomwa mahakamani kuwa ni Jabir Ali Dzuya, Bwana mkuu Alwan Jabu, na Antony Mwatela Mughendi.

Hakimu mkazi Martin Muya ameagiza washukiwa wachunguzwe kiafya, na kuzuiliwa rumande kabla ya kesi hiyo kuendelea kusikizwa.