Papa Benedict ajiuzulu rasmi.

Papa Benedict akisalimia waumini alipokuwa akiwasili St.Peters Square .

Papa Benedict amejiuzulu baada ya karibu miaka minane madarakani na kuwa kiongozi wa kwanza wa kanisa katoliki kuachia madaraka kwa hiari baada ya kipindi cha miaka 600.

Kujiuzulu kwa Papa Benedict kulianza rasmi alhamisi saa mbili usiku saa kadhaa baada ya kuondoka Vatikan kwa helikopta na kuelekea kwenye eneo la mapumziko la Papa la Castel Gandofo nje ya Rome. Ilipofikia muda huo walinzi wawili wa Swiss Guard waliokuwa wakilinda lango kuu kwenye nyumba ya Papa walifunga mlango mkuu na kuondoka .

Mapema siku hiyo kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 85 aliahidi heshima ya hali ya juu kwa mrithi wake wakati akizungumza na makardinali wa kanisa katoliki katika hafla ya faragha ya kumwaga huko Vatikan. Aliwataka kuungana akisema kati yenu yuko Papa ajaye ambae itabidi wamchague katika wiki zijazo.