Mamilioni ya watu ulimwenguni wanaathiriwa na matatizo ya afya ya akili. Shirika la Afya Duniani (WHO) linaripoti watu wenye matatizo ya akili ni takriban asilimia 13 ya mzigo wa maradhi duniani, na theluthi moja ya magonjwa yanayohusishwa na ulemavu.
Tafiti zilizofanywa nchini Marekani, Uingereza na Ethiopia zinaonyesha kuwa watu wenye matatizo makubwa ya maradhi ya akili wanafariki miaka 10 mpaka 20 mapema kuliko watu wengine kwa ujumla. Mratibu wa Afya ya Akili katika WHO, Michelle Funk anasema watu wenye matatizo ya akili mara nyingi hutengwa na kupuuzwa.
Anasema huduma wanazopatiwa kwa hali walizonazo kwa ujumla hazitoshi na mara nyingi ni mbaya kote ulimwenguni. Bi Funk anasema wananyimwa haki za msingi na kuvuliwa utu wao, mambo ambayo muhimu sana kwa wao kuweza kupata nafuu.
"Tunachokiona badala yake ni kwamba wanalazwa katika mahospitali kwenye nchi zote duniani na wanajikuta wakikabiliwa na ghasia na manyanyaso ya kingono. Wanazuiliwa. Wanafungwa kamba. Wanaachwa bila ya chakula na maji, na kulazimishwa kuishi katika maeneo machafu sana na hali ambayo si nzuri kiafya, kwa ujumla wanasahauliwa kwa miaka kadhaa na mara nyingine maisha yao yote," anasema Bi Funk.
WHO inasema huduma duni za afya zinatokana na ukosefu wa wafanyakazi wa afya wenye ujuzi na hali mbaya kwenye maeneo wanayowekwa jambo ambalo linapelekea ukiukaji zaidi wa haki zao. WHO inaendesha kampeni za kuwaelimisha watu ambazo zinawalenga kuondokana na dhana nyingi na mawazo potofu kuhusu ugonjwa wa akili.