Mapigano nchini Sudan yaliendelea kwa siku ya pili Jumapili katika mapambano kati ya majenerali hasimu waliotwaa madaraka katika mapinduzi ya mwaka 2021 na kusababisha vifo vya zaidi ya raia 50 wakiwemo wafanyakazi watatu wa Umoja wa Mataifa na kuzua taharuki kimataifa.
Milipuko ya mizito na milio mikali ya risasi ilitikisa majengo katika mji mkuu Khartoum wenye idadi kubwa ya watu kaskazini na kusini mwa nchi huku vifaru vikiwa vimejaa mitaani na ndege za kivita zikiruka angani walioshuhudia wamesema.
Ghasia zilizuka mapema Jumamosi baada ya wiki kadhaa za mapambano ya madaraka kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan, na naibu wake Mohamed Hamdan Daglo, kamanda wa vikosi vyenye silaha nzito Rapid Support Forces (RSF) huku kila mmoja akimshutumu mwenzake kwa kuanzisha mapambano hayo.
Milio ya risasi na milipuko inaendelea, alisema Ahmed Hamid mwenye umri wa miaka 34 kutoka kitongoji cha kaskazini mwa Khartoum. Hali ni ya kutia wasiwasi sana na haionekani kama itatulia hivi karibuni alisema Ahmed Seif mkazi mwingine wa Khartoum ambaye anahofu jengo lake liliharibiwa na milio ya risasi lakini alisema ilikuwa hatari sana kwenda nje kuangalia.
Pande zote mbili zinadai kudhibiti maeneo muhimu huku televisheni ya taifa ikitangaza nyimbo za uzalendo bila kutoa maoni.