Watu wasiopungua 10 wameuawa Jumatano katika mji wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC mjini Goma baada ya wanajeshi walipojaribu kuzuia maandamano ya kundi la kidini dhidi ya Umoja wa Mataifa, waandaaji na maafisa wa hospitali wamesema.
Moleka Maregane, mwanachama wa kundi la Natural Judaic and Messianic Faith towards the Nations, lililoandaa maandamano hayo alisema wanajeshi wa Congo waliwaua watu sita katika kituo cha redio na nyumba ya ibada mapema asubuhi, kabla ya maandamano hayo kufanyika.
Meya wa mji wa Goma, Kanali Faustin Napenda Kapend pia ameliambia shirika la habari la AFP kwamba polisi mmoja alitekwa na waumini wa kundi hilo la kidini. Vikosi vya usalama vilichoma moto hekalu la kundi hilo, aliongeza. Maafisa wa hospitali wamesema wamewapokea majeruhi 33, watatu kati yao walifariki kutokana na majeraha.
Msemaji wa jeshi la Congo katika jimbo la Kivu Kaskazini, Luteni Kanali Guillaume Ndjike, amesema watu 20 wamekamatwa. Watu hawa wanacheza mchezo wa adui na wanatumiwa na pia wametumia dawa za kulevya, alisema katika taarifa iliyorekodiwa.
Forum