Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 22:16

Wasifu wa mgombea nafasi ya urais Henry Tumukunde


Mgombea urais Henry Tumukunde
Mgombea urais Henry Tumukunde

Henry Tumukunde ni afisa wa jeshi mstaafu katika jeshi la Uganda Peoples Defence Forces – UPDF.

Alikuwa waziri wa usalama wa kitaifa kati ya June 6 2016 na March 4 2018 kabla ya kufutwa kazi na baadaye kutangaza kugombea urais.

Tumukunde, ambaye ni wakili, alisimamia kuandikishwa na utendakazi wa wanajeshi pamoja na ujasusi na kuwa kamanda wa ngazi ya nne wilayani Gulu, kaskazini mwa Uganda.

Alikuwa pia mkuu wa usalama wa ndani wa Uganda na mbunge aliyewakilisha wanajeshi katika bunge la sita na saba, kati ya mwaka 1996 na 2005.

Henry Tumukunde alizaliwa Februari 28, 1959 katika wilaya ya Rukungiri, magharibi mwa Uganda. Alisomea katika shule ya msingi ya Bishop Stuart, shule ya upili ya Kigezi na katika shule ya upili ya Kibuli.

Amesoma sheria katika chuo kikuu cha Makerere ambapo alimaliza masomo yake mwaka 1981 kabla ya kujiunga katika vita vilivyokuwa vinaongozwa na Yoweri Museveni ambavyo vilimuingiza maadarakani miaka 5 baadaye.

Ana shahada ya uzamili katika usimamizi wa maswala ya mafuta na gesi kutoka chuo cha elimu ya juu cha Geneva, mwaka 2013.

Kujiunga katika vita vilivyoongozwa na Museveni

Jeshi la Wananchi wa Uganda
Jeshi la Wananchi wa Uganda

Wakati alikuwa akisoma katika chuo kikuu cha Makerere, Tumukunde alijihusisha sana na siasa za kupinga serikali ambazo zilipelekea kijiunga na waasi waliokuwa wakipigana katika eneo la Luweero dhidi ya serikali ya rais Milton Obote.

Tumukunde aliungana na meja Generali Mugisha Munt una kanali Jet Mwebaze.

Alipanda ngazi katika kundi hilo la waasi na kuwa mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu.

Alipigwa risasi mara kadhaa miguuni wakati wa vita lakini akanusurika kifo, japo inaripotiwa kwamba makamanda wenzake walikuwa wamepoteza matumaini iwapo angepona.

Alisafirishwa kisiri hadi jijini Nairobi Kenya kwa matibabu, na baadaye hadi London ambapo alifanyiwa upasuaji maalum na kupona.

Museveni alipoingia madarakani mwaka 1986, alimpandisha Tumukunde cheo katika jeshi na kuwa Major, pamoja na kuwa kiongozi wa kwanza wa shughuli za kijeshi katika ubalozi wa Uganda nchini Uingereza.

Baadaye, alipelekwa kwa mafunzo maalum ya kijeshi nchini Nigeria ambapo alikuwa mmoja wa wanafunzi bora zaidi.

Alirejea Uganda na kuteuliwa kuwa mkuu wa mipango yote ya jeshi la Uganda.


Tumukunde katika siasa

Mnamo mwaka 1994, Tumukunde alichaguliwa kuwakilisha eneo la Rubabo katika baraza la kuandika katiba ya Uganda ya mwaka 1995.

Alipandishwa cheo katika jeshi na kuwa Lieutenant colonel kabla ya kuoandishwa tena cheo mwaka 1998 na kuwa colonel Pamoja na mkuu wa ujasusi katika jeshi.

Alipandishwa tena cheo na kuwa Brigedier na kuwa kamanda wa kikosi cha nne cha jeshi la UPDF wilayani Gulu wakati waasi wa Lords resistance Army walikuwa wanapigana dhidi ya utawala war ais Yoweri Museveni.

Alikuwa Gulu kwa mda mfupi kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa ujasusi nchini Uganda.

Kupinga mabadiliko ya katiba kinyume na msimamo wa museveni

Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni

Mnamo mwaka 2003, Tumukunde mbele ya rais Museveni na baraza lake la mawaziri alipinga hatua ya Museveni kutaka kubadilisha katiba na kuondoa ukomo wa mihula kwa rais, katika hatua ya kutaka kuendelea kuongoza bila kikomo.

Tumukunde alisema kwamba hatua hiyo ilikuwa kinyume na sababu zilizofanya Museveni na wenzake kuanza vita kuondoa utawala uliokuwepo madarakani kabla yam waka 1986.

Hatua hii, ilipelekea Tukunde kuwa katika uhusiano mbaya na Museveni.

Baadaye alifunguliwa mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kueneza habari potofu ambazo ni hatari kwa utawala wa Museveni. Mashtaka hayo yalitupiliwa mbali na mahakama ya kijeshi.

Alilazimika kujiuzulu kiti chake cha bunge kama mwakilishi wa jeshi mwaka 2005.

Alikamatwa baadae na kuhukumiwa na mahakama ya kijeshi mwaka 2010 kwa makosa ya kukiuka sheria za jeshi la Uganda lakini akaachiliwa huru baadae.

Alipandishwa cheo mwaka 2015 na kufikia ngazi ya Lieutenant General kabla ya kustaafu kutoka jeshi.

Mwaka mmoja baadaye, Museveni alimteua kuwa waziri wa usalama. Alifutwa kazi hiyo March 2018, pamoja na aliyekuwa mkuu wa polisi Generali Kale Kayihura.

Mgombea wa urais

Tangu alipotangaza kugombea urais nchini Uganda Lt. Gen. Henry Tumukunde amekuwa akijadiliwa sana nchini humo.

Katika barua aliyoandikia tume ya uchaguzi Februari 28 mwaka huu, alisema kwamba lengo lake la kugombea kiti cha rais ni “kuleta mabadiliko ambayo waliahidi Uganda walipoenda msituni kupigana utawala uliokuwepo kabla ya Museveni na kupokeza madaraka kwa njia ya amani kutoka utawala mmoja hadi mwingine.”

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG