Vikosi maalum vya Marekani vilifanikiwa kuwahamisha wanadiplomasia wa Marekani na familia zao kutoka ubalozi wa Marekani mjini Khartoum mapema Jumapili. Operesheni hiyo ilichukua chini ya saa moja, maafisa walisema.
Ufaransa ilitangaza baadaye Jumapili kwamba inawahamisha pia wafanyakazi wake wa kidiplomasia kutoka Khartoum. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema katika taarifa Jumamosi jioni kwamba shughuli katika ubalozi wa Khartoum zimesitishwa kwa muda.
Blinken alisema alielekeza kufungwa kwa muda kwa ubalozi huo kwa sababu ya hatari kubwa na inayoongezeka ya usalama iliyosababishwa na mzozo kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na Rapid Support Forces ambao umesababisha idadi kubwa ya vifo vya raia pamoja na majeruhi ilisema taarifa hiyo.
Rais Joe Biden katika taarifa yake Jumamosi jioni alisema zoezi la kuwaondoa watu limekamilika na anawashukuru wanajeshi wa Marekani waliofanya operesheni hiyo. “Ninajivunia kujitolea kwa kipekee kwa wafanyakazi wetu wa ubalozi ambao walifanya majukumu yao kwa ujasiri na weledi na kujumuisha urafiki na uhusiano wa Marekani na watu wa Sudan, Biden alisema. “Ninashukuru kwa ustadi usio na kifani wa wahudumu wetu ambao walifanikiwa kuwafikisha salama.”
Rais Biden pia aliishukuru nchi ya Djibouti, Ethiopia na Saudi Arabia ambapo alisema wamefanya jukumu kubwa muhimu katika mafanikio ya operesheni yetu”. Kiasi cha wamarekani 70 walisafirishwa kwa ndege kutoka ubalozi wa Marekani mjini Khartoum kwenda Ethiopia maafisa walisema. Wafanyakazi wenzao wa kidiplomasia kutoka balozi nyingine ambao walikuwa katika ubalozi wa Marekani wakati ndege ilipowasili pia walijumuishwa katika operesheni hiyo ya ndege afisa mmoja alisema.
Biden alitoa agizo hilo walisema baada ya kupokea tathmini Jumamosi kutoka kwa washauri wa usalama wa taifa kwamba mapigano hayatapungua.