Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 05:57

Vyanzo na suluhisho la ajali za barabarani Afrika Mashariki


Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa ajali nyingi za barabarani, katika ukanda wa Afrika Mashariki, zinatokana na kutofuatwa kwa sheria za barabarani,

Kwa mujibu wa taarifa hizo madereva wasio na weledi na kitendo cha kutozingatiwa maswala ya kiusalama kwa vyombo vya usafirishaji ndio vyanzo vikuu vya ajali hizo.

Karibu kila nchi ya Afrika Mashariki ina sheria nzuri za vyombo vya usafirishaji lakini rushwa hufunika sheria.

Ripoti ya Shirika la Afya duniani (WHO) inabainisha kwamba nchi nyingi zimeboresha sheria kama vile kuzuia mwendo kasi, ulevi na matumizi ya vifaa vya usalama kama matumizi ya mikanda, kofia za bodaboda yaani Helmet na hata viti maalumu kwa watoto.

Sospeter Mziwanda ni dereva wa mabasi ya Shabiby nchini Tanzania anasema;

“Sababu za ajali zipo nyingi lakini kwa uchache ni ufinyu wa barabara, mwendo kasi na uzembe wenyewe wa madereva hasa ikizingatiwe wengi wao hawana elimu ya kutosha ya udereva.”

Pamoja na barabara nyingi za Afrika Mashariki kuelezwa kuwa ni nyembaba na mbovu zisizotoa mwanya wa makosa kwa madereva, WHO ilipendekeza mwendo kasi wa kutumika barani Afrika. Imependekeza mwendo kasi wa juu usiozidi kilometa 50 kwa saa, lakini inadaiwa nchi 47, zinazowakilisha watu milioni 950, zinaheshimu mapendekezo hayo.

Uganda ni kinara wa ajali za barabarani kwa ukanda wa Afrika Mashariki. Inadaiwa mwendo kasi uliopitiliza, barabara mbovu na ulevi ndivyo vyanzo vikuu vya ajali za barabarani kama anayoeleza Akor Amazima mchambuzi wa masuala ya kijamii nchini Uganda.

“Vyanzo vya ajali za barabarani nchini Uganda vipo vingi sana, lakini tatizo la ushirikina, barabara kuwa mbovu, barabara kuwa nyembamba sana, vilevile madereva wanaendesha bila kujali maisha ya watu, na magari mabovu, ikijumuisha usimamizi mbaya, lakini pia watembea kwa miguu nao wanachangia ajali za barabarani.”

Nchi za Afrika Mashariki zina sheria za barabarani ambazo katika maandishi huonekana nzuri, japo wadau wa usafirishaji wakisema sio kali kama ilivyo katika nchi nyingine. Kama anavyoeleza dereva Sospeter Mziwanda:

“Zipo nchi zenye sheria kali kidogo hasa kwa madereva wa mabasi, mfano niliwahi kwenda Angola, nikakuta masharti ni magumu, hata Rwanda pia ni magumu na ndio maana uzembe kwa madereva kule ni mdogo kuliko kwetu.”

Taarifa rasmi za idara za usalama barabarani za Afrika Mashariki, zinaeleza vyanzo vya ajali vinavyo shabihiana ni makosa ya kibinadamu, hasa uzembe wa madereva, kutotii sheria na kanuni za barabarani, mwendo kasi, matumizi ya vileo, ubovu wa barabara na ubovu wa vyombo vya usafiri vyenyewe.

Lakini wananchi wenyewe wanakubaliana na haya? Abdallah Nyambo ni mkazi wa nchini Kenya na anasema.

“Ajali zinatokana na wamiliki kutozingatia sheria kwa mfano wanajaza sana, na ufisadi kuuingizwa katika uendeshaji wa biashara nzima, hongo kwa wanausalama, unakuta gari linakimbia sana na hawafanyi chochote.”

Wataalamu wanasema ajali nyingi za barabarani zinaepukika. Tanzania inayokabiliwa na kiwango kikubwa cha ajali za barabarani imeweka kanuni nyingi mpya za kupunguza ajali hizo, baadhi yake ni umri.

Dereva wa mabasi ya mijini atatakiwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 60. Mabasi ya shule na yanayosafiri masafa ya mbali madereva wake wanatakiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 60. Yule atakayeendesha zaidi ya saa nane atatakiwa kuwa na msaidizi.

Kwa upande wa viwango vya adhabu navyo vimepandishwa licha ya kuzua mjadala mkubwa. Hayo yote pia yamefanyika kwa namna nyingine nchini Kenya, na Uganda, lengo likiwa ni kupunguza ajali za barabarani.

Nchini Uganda imetajwa kampeni ya nenda salama kuwa ni mojawapo. Hali ya kampeni ndani ya magari ipo pia kwa vyombo vya usafiri vya umma nchini Kenya.

Lakini pamoja na juhudi nyingi za kupunguza ajali za barabarani, ukanda huo bado una changamoto kubwa ya kushughulikia usafiri wa pikipiki maarufu kama boda boda. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita nchi za Afrika Mashariki zimeshuhudia ongezeko kubwa la usafiri huu unaoendeshwa na vijana wengi wasiokuwa na elimu ya usalama barabarani wala leseni.

XS
SM
MD
LG