Viongozi kutoka karibu mataifa 140 wanaohudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kutathmini maendeleo yaliyopatikana katika Malengo ya Maendeleo ya Milenia, MDG’s wanaendelea kuhimiza kufikia malengo hayo bila ya kulalamika dhidi ya matatizo ya kiuchumi.
Mnamo siku ya pili ya mkutano mjini New York, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alitoa wito kwa viongozi wa dunia kuendelea kufanya kazi kutekeleza malengo yaliyowekwa miaka 10 iliyopita.
Alisema jukumu la msingi la maendeleo lingali liko mikononi mwa serikali za nchi zinazoendelea, akisema serikali hizo zinahitaji kuimarisha utawala bora.
Rais Mahmoud Ahmadinejad alilaumu ubebari na mashirika ya biashara ya kimataifa kwa matatizo kote duniani.
ais Robert Mugabe wa Zibabwe alilaani pia siku ya Jumanne vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi yake na washirika wake wa karibu. Alieleza vikwazo kua vipingamizi vinavyoumiza maendeleo ya Zimbabwe.
Moja kati ya malengo yanayokabiliwa na changamoto kubwa ni lengo la 6, la kupambana na HIV ukimwi, malaria na magonjwa mengine ya kuambukiza.
Kila siku zaidi ya watu 7 400 kote duniani wanaambukizwa na virusi vya HIV vinavyo sababisha ugonjwa wa ukimwi. Kote duniani kuna watu milioni 33 wanaoishi na virusi hivyo, theluthi mbili kati yao wako afrika kusini mwa jangwa la sahara.
Lakini mkuu wa idara ya ukimwi ya Umoja wa Mataifa UNAIDS Bw. Michele Sidibe anasema licha ya idadi hiyo kubwa kumekuwepo na maendeleo muhimu yaliyopatikana katika vita dhidi ya janga hili.
"Kwa mara ya kwanza tumeweza kupunguza uambukizaji mpya kwa asili mia 25 katika mataifa 22 yeneye uambukizaji mkubwa kabisa huko Afrika. Hii ni muhimu kwa sababu si jambo la kupunguza idadi ya watu tu katika kuambukizwa upya, bali inapunguza pia gharama za matibabu kwa sababu wanaohitaji tiba wanapunguka”, amesema Bw Sidibe.
Baadhi ya mataifa yenye idadi kubwa ya watu waloambukizwa ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini Zimbabwe na Nigeria zinaongoza katika kupunguza uambukizaji. Hali hii ni muhimu kwani malengo ya maendeleo ya mileni yanaingiliana kwa mfano vita dhidi ya HIV na Ukimwi inambatana na kupunguza vifo wakati wa kujifunguwa akina mama ikiwa ni lengo la tano la MDGS.