Timu ya Ureno, Jumatano ilianza mazoezi makali kujiandaa na mchezo wa raundi ya pili na Uruguay ambayo ilifuzu raundi ya pili kwa kushinda michezo yote ya kundi A.
Ikiwa na mwanasoka bora wa dunia mwaka huu Christiano Ronaldo, Ureno itapambana na Uruguay inayoundwa na wachezaji wenye uzoefu akiwemo Luis Suarez.
Ronaldo na wachezaji waliocheza katika mchezo wa mwisho na Iran, walihudhuria mazoezi yao katika kambi iliyopo mjini Kratovo. Mlinzi wa Ureno, Cedric Soares akiwa mazoezini amesema Uruguay ni timu nzuri lakini ameahidi kupambana katika mchezo wao.
Katika hatua nyingine, nahodha wa Argentina, Lionel Messi amesema hakutarajia upinzani mkali dhidi ya Nigeria. Ilibidi kusubiri mpaka dakika ya 86 kwa Argentina kupata goli la ushindi.
Akiongea na wanahabari, Messi amesema walijiamini watashinda na kupata nafasi katika 16 bora za Kombe la Dunia Russia 2018. Ushindi wa goli 2-1 umeikutanisha Argentina na Ufaransa katika mchezo wa mtoano.
Messi ambaye ametimiza miaka 31 wiki hii, amesema ushindi wa Nigeria wa 2-0 dhidi ya Iceland uliwachochea kutetea nafasi ya kuendelea na mashindano baada ya kufungwa na Croatia 3-0, na awali kutoka suluhu na Iceland ya 1-1.
Katika mchezo wa Argentina na Nigeria, Diego Maradona mwanasoka nguli wa zamani kutoka Argentina alionekana akifanya vituko. Jumatano amesema alipigwa faini kwa kuonyesha ishara isiyo kubalika katika mchezo wa Argentina na Nigeria.
Baada ya mchezo, Maradona alionekana akisindikizwa na watu ikidaiwa alipatwa na matatizo ya kiafya. Akiwa na umri wa miaka 57 sasa, Maradona alitumia ukurasa wake wa Instagram, kueleza ni mzima wa afya na hakupelekwa hospitali.
Wakati wa mchezo huo, Maradona alisababisha umma kumfuatilia kutokana na vituko alivyokuwa akivifanya jukwaani wakati Argentina ikijiokoa kutolewa katika Kombe la Dunia Russia 2018.