Hakuna eneo jingine la dunia ambalo lina watu wengi wanaoishi na virusi vya HIV au limewahi kufiwa na watu wengi kutokana na Ukimwi kuliko bara la Afrika. Hata hivyo, licha ya kuwa kitovu cha matatizo yanayohusiana na ugonjwa huo, miaka mingi ilipita bila watu kuhamasishwa kuuhusu, na muda mrefu zaidi kwa wagonjwa kupokea dawa za kuokoa maisha kwa bei ambayo wangemudu.
Miaka ya kwanza ya Ukimwi barani Afrika, ugonjwa huo haukuwa na jina rasmi. Katika maeneo mengi, uliitwa ugonjwa wa kukonda kwa maana watu walikondeana kabla ya kufariki. Haukuua watu wachanga au wazee kwa wingi, lakini uliangamiza waliotegemewa kuchumia familia zao riziki ya kila siku, walimu, wakulima, mama na baba wazazi - watu wa umri wa makamo.
Ghafla, wazee wa miaka zaidi ya themanini walijipata wakilea wajukuu walioachwa na watoto wao.Unyanyapaa, ubaguzi na itikadi duni zilikita mizizi. Ukosefu wa habari kuhusu virusi vya HIV - upungufu ambao ulikita hata serikalini - ulisababisha vifo vya wengi.
Mamilioni ya watu walikufa kutokana na Ukimwi Afrika.Daktari Thomas Frieden mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Maradhi (CDC) cha Marekani anasema:
"Janga la Ukimwi lilipofikia kileleni barani Afrika, lilisababisha theluthi mbili za vifo vyote vya watu wazima vilivyotokea kote barani. Hebu tafakari hali hiyo ingekuwaje katika kijiji chetu binafsi, jamii yetu binafsi. Kuna jamii ambazo biashara iliyonoga zaidi wakati huo ilikuwa ya mazishi tu."
Wananchi wa tabaka lisilojaaliwa sana kimaisha walijipata wakikabiliwa zaidi na janga la Ukimwi, wakawa viongozi na wanaharakati. Miongoni mwa wanaharakati walioibuka kutokana na hali hiyo ni Noerine Kaleeba, mmoja wa wahamasishaji wakuu nchini Uganda - la labda kote barani Afrika - wanaojulikana zaidi kwa kuzindua na kuhamasisha watu kuhusu ugonjwa huo.
Alianza kuona ithibati za maafa ya Ukimwi akihudumu katika hospitali mnamo 1983. Kaleeba anasema,
"Ni wakati huo ambapo nadhani Uganda ilianza kugundua kwa hakika kwamba tulikuwa tukipuuza janga ambalo lazima lingetokea."
Alilojua tu wakati huo, anasema, ni kwamba ugonjwa uliotokana na virusi ulikuwa ukisambaa, na hasa miongoni mwa makahaba. Kaleeba aliona mwanamume mchanga katika hospitali alikohudumu aliyedhoofishwa na ugonjwa huo.
Alichukulia aliyoona jinsi watu wengi walivyochukulia wagonjwa wa Ukimwi wakati huo. Kaleeba anaelezea hofu yake.
“Niliingiwa na hofu sana kuhusu maisha yangu binafsi. Sikumgusa mgonjwa huyo. Lakini mwaka mmoja baadaye mume wangu binafsi aligunduliwa kuwa na Ukimwi.”
Huo ulikuwa mwaka wa ’86 na ghafla Kaleeba na familia yake ilijikuta katikati ya janga la Ukimwi. Mumewe Christopher aligunduliwa kuwa katika hatua za mwisho mwisho za athari sugu za Ukimwi akiwa mwanafunzi nchini Uingereza. Kaleeba alifahamishwa kuhusu hali ya mumewe kwa njia ya telegram iliyotoka kwa serikali ya Uingereza. Kaleeba hakuamini alichosikia.
“Mwanzo sikuamini nilipopata ujumbe huo kwa sababu nilijua kuhusu Ukimwi kwamba wakati huo ulikuwa ugonjwa unaoambukiza watu wabaya.. watu wanaofanya ngono za kiholela. Na nilijua kwa uhakika kuwa mimi wala mume wangu hatukuwa miongoni mwa watu waliofanya ngono za kiholela.” Labda aliyezua ubishi mkuu zaidi kuhusu ugonjwa huu ni aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki aliyeshikilia kuwa Ukimwi hausababishwi na virusi pekee. Wanasayansi wengi walitia saini Maazimio ya Durban yaliyomhimiza akubali ushahidi kwamba virusi ndivyo chanzo cha Ukimwi. Rais huyo alisema:
"Nilioneleakwamba hatungechukulia kuwa chanzo cha Ukimwi ni virusi pekee. Pia, nilionelea kwamba kila Mwafrika aliye hai, ama ana afya au anaugua, anakabiliwa na maadui wengi wa afya ambao wangetangamana kwa njia mbalimbali mwilini mwake."
Wanaharakati na wanasayansi wengi husema msimamo wa Bwana Mbeki ulichelewesha huduma muhimu na matibabu, hali iliyosababisha vifo vya watu wengi. Kongamano la Durban pia lilishughulikia suala la mayatima wanaofiwa na wazazi kutokana na Ukimwi.
Ilitabiriwa kwamba janga hili lingeacha watoto wengi wakiwa mayatima.Watoto wengi walizungumza katika kongamano hilo, miongoni mwao msichana huyu wa miaka kumi na miwili.
"Sikujua kwamba mama yangu alikuwa na virusi vya HIV. Niliishi naye bila kujua mambo hayo yote, halafu akafa. Kwangu ilikuwa vigumu sana kukua bila mama, na baba yangu alikuwa amefariki miaka mingi iliyopita. Na sasa ndugu yangu, hata yeye pia anakaribia kufa na sijui nifanye nini.”
Mashirika mengi yalianzishwa ili kusaidia mayatima, miongoni mwayo lile la Nyumbani nchini Kenya na Wakfu wa FXB.Sasa kuna ongezeko la kupatikana kwa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi Afrika hasa kwa hisani ya Mpango wa Rais wa Marekani wa Msaada wa Dharura wa Ukimwi (PEPFAR),
Hazina ya Dunia ya Kukabili Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, na Wakfu wa Clinton. Lakini ni makabiliano marefu na magumu ya kisheria yaliyofanyika Afrika Kusini ambayo yalifungua mlango. Mnamo 2001, katika kesi kubwa ya kihistoria, takribani kampuni arobaini za dawa ziliacha kupinga sheria iliyoruhusu dawa za bei nafuu za Ukimwi kuuzwa.
Kongamano la Kimataifa la Ukimwi, ambalo ndilo kubwa zaidi kuhusu ugonjwa huo kuwahi kuandaliwa, litafanyika jijini Washington, D.C., hapa Marekani, kuanzia Julai 22 hadi Julai 27 mwaka huu wa 2012.