Vyombo vya usalama nchini Ujerumani vimemtia nguvuni raia wa Tunisia anayedaiwa kuwa na uhusiano na Anis Amri aliyehusika na shambulizi la kinyama katika soko la krismasi mjini Berlin.
Waendesha mashtaka wamesema Jumatano kuwa mtu huyu mwenye umri wa miaka 40 alikamatwa baada ya msako uliofanyika katika sehemu ya biashara na nyumbani kwake. Maafisa hao wamesema nambari ya simu ya mtu huyu ilipatikana katika simu ya mkononi ya Amri.
“Uchunguzi unaonyesha kuwa Mtunisia huyu inawezekana alikuwa na mahusiano na mshambuliaji,” mwendesha mashtaka wa shirikisho alisema katika taarifa.
Waendesha mashtaka wana muda mpaka Alhamisi kuamua kama wana ushahidi wa kutosha au hapana ili kuomba hati rasmi ya kumkamata.
Amri alitumia lori kuvamia ndani ya soko lililokuwa limejaa watu, na kuua watu 12 na kujeruhi wengine 56. Kabla ya kufanya shambulizi hilo alitengeneza video ambayo ilionyesha anakula kiapo kushirikiana na kundi la kigaidi la Islamic State na kiongozi wao, Abu Bakr al-Baghdadi.
Baada ya kuhamia kinyemela kutoka Tunisia mwaka 2011, Amri alitumikia kifungo kwa kosa la kuchoma moto kituo cha makazi ya wakimbizi nchini Italy. Alipoachiwa hatua za kumrudisha Tunisia zilishindikana kutokana na sababu mbali mbali.
Baadae alisafiri mpaka Uswizi na kisha Ujerumani, ambapo inaelekea alighilibiwa na mtandao wa watu wenye msimamo mkali ambao wanatuhumiwa kuwa ni wenye kuwaingiza vijana katika kundi la Islamic State.
Ingawa Ujerumaniilim,nyima hifadhi mapema mwaka huu na kuonyesha kuwa ni mwenye dalili za tishio la ugaidi, vyombo vya usalama vilivuta subira kungojea mchakato wa kupokea makaratasi ya kumrudisha Tunisia.
Wakati tu taratibu za kumrudisha zikikamilishwa, Amri anasadikiwa kuwa aliteka lori na kuliendesha kwa kasi kubwa ndani ya soko la krismasi la Berlin lilokuwa limefurika watu.
Amri alipigwa risasi na polisi wa Italy katika kituo cha treni mjini Milan.