Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:24

Uganda imeanza kuilipa DRC fidia kwa ajili ya uvamizi mashariki mwa nchi hiyo miaka 20 iliyopita


Mkongo akitizama uharibifu uliofanyika katika mtaa wa Tshopo mjini Kisangani badaa ya wanajeshi wa Rwanda kuwashinda wanajeshi wa Uganda Juni 11 2000.
Mkongo akitizama uharibifu uliofanyika katika mtaa wa Tshopo mjini Kisangani badaa ya wanajeshi wa Rwanda kuwashinda wanajeshi wa Uganda Juni 11 2000.

Waziri wa Sheria wa Jamhuri ya Kidemkorasia ya Kongo anasema Uganda imeanza kuilipa Kinshasa fidia ya dola milioni 65 kati ya 325 kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Sheria ya Kimataifa ICJ

Kulingana na maafisa wa serikali mjini Kinshasa waliozungumza Jumamosi, ni kwamba waziri wa sheria Rose Mutombo aliliarifu Baraza la Mawaziri siku ya Ijumaa kuwa Uganda imeanza kulipa fidia na riba baada ya ICJ kuikuta na hatia ya uvamizi wa mashariki mwa Congo miaka 20 iliyopita.

Bi Mutombo ameliambia baraza kwamba kulingana na makubaliano Uganda itailipa Congo fedha zote kwa awamu tano ikiwa ni dola milioni 65 kila mwaka, ambapo malipo ya kwanza yametolewa Septemba 1, 2022.

Baada ya mivutano ya kisheria ya muda mrefu, Mahakama ya Sheria ya Kimataifa, chombo kikuu cha sheria cha Umoja wa Mataifa, hapo Februari 10 mwaka 2022, kilifikia uamuzi wa kuitaka Kampala kuilipa Kinshasa dola milioni 325 kwa kuivamia Congo wakati wa vita vyake vya pili, kati ya 1998 hadi 2003.

Kiwango hicho cha fedha ni kidogo sana kulingana na dola bilioni 11 ambazo DRC imekua ikidai, ingawa Uganda imeichukulia hukumu hiyo haikuwa ya haki, na wamesikitishwa kwamba uamuzi ulichukuliwa wakati nchi hizo mbili zilikuwa zinaendelea kuimarisha uhusiano kati yao.

Waziri wa Sheria ameliambia baraza la mawaziri kwamba fedha zilizolipwa na Uganda zitawekwa katika akaunti ya muda ya wizara ya sheria, katika benki ya Congo, na fedha hizo haziwezi kutumiwa hadi zimelipwa kwa ukamilifu na kutumiwa kwa ajili ya mfuko maalum kuwalipa fidia waathirika.

Ilipokuwa inatoa uamuzi wake mahakama ya ICJ ilieleza kwamba kati ya dola milioni 325, ni dola 225 zitakazotumiwa kuzilipa familia za waliouawa, na dola milioni 40 kulipa hasara za mali na milioni 60 fidia kwa mali asili iliyopotea.

XS
SM
MD
LG