Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 09:55

Timu ya Cameroon yatoa dola 85,000 kwa waathirika wa mkanyagano


Wachezaji wa Cameroon wakiwa katika muda wa ukimya kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa mkanyagano, kabla ya kuanza kwa michuano ya robo fainali katika Kombe la Mataifa ya Afrika 2022
, Jan. 29, 2022.
Wachezaji wa Cameroon wakiwa katika muda wa ukimya kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga wa mkanyagano, kabla ya kuanza kwa michuano ya robo fainali katika Kombe la Mataifa ya Afrika 2022 , Jan. 29, 2022.

Timu ya taifa ya Cameroon, Indomitable Lions, Jumapili ilitoa dola 85,000 na kujitolea ushindi wao wa bao 2-0 dhidi ya Scorpions ya Gambia kwa waathirika wa mkanyagano ulioua watu wanane na kujeruhi 38 kwenye uwanja wa Yaoundé wa Olembe wiki hii.

Maafisa wa timu ya taifa ya Cameroon, Indomitable Lions, wanasema kwamba Mungu atawabariki waathirika wa janga la juma lililopita kwenye uwanja wa Yaoundé wa Olembe. Wachezaji hao waliimba Jumamosi jioni huko Douala, kitovu cha uchumi cha Cameroon na mji wa pwani, baada ya kuwafunga Scorpions ya Gambia katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON.

Taarifa baada ya mechi hiyo kutoka kwa Serge Guiffo, afisa habari wa Indomitable Lions, ilisema wachezaji hao wametoa dola 85,000 na kujitolea ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya Scorpions ya Gambia kwa waathirika wa ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu nane na kujeruhi wengine 38.

Taarifa hiyo haikueleza jinsi fedha hizo zitakavyogawiwa kwa waathirika, lakini ilisema wanafamilia wa waliofariki katika mkanyagano huo watapewa sehemu ya fedha hizo.

Narcisse Mouelle Kombi, waziri wa michezo na elimu ya viungo wa Cameroon , aliwahutubia wachezaji kwenye uwanja wa Japoma mjini Douala baada ya mechi.

Kombi anasema Wacameroon wana furaha kwamba wachezaji wao wa timu ya taifa wamewasaidia watu waliofariki au kujeruhiwa wakati wakijaribu kutazama Indomitable Lions walipokuwa wakicheza. Anasema raia wa Cameroon wana furaha kwamba mchango huo unakuja baada ya ushindi wa kihistoria dhidi ya Scorpions ya Gambia.

Mshtuko huo ulitokea huku umati wa watu wakihangaika kuingia Uwanja wa Olembe mjini Yaoundé. Rais wa Cameroon Paul Biya aliamuru waliojeruhiwa kutibiwa bila malipo.

Ndukong Edward, mwanafamilia wa muathirika wa mkanyagano, anasema rais hakutoa tamko kuhusu msaada wowote kwa familia za waathirika waliokufa. Ndukong anasema anatumai serikali itawasaidia waliojeruhiwa na wanafamilia wa waliofariki. Anasema kulegalega kwa usalama na polisi wa Cameroon inawezekana kumesababisha mkanyagano.

Anasema kama lango lingefunguliwa jinsi ilivyotakiwa, hakuna kitu ambacho kingefanyika kwa sababu watu wangeingia uwanjani. Lakini ikiwa lango hilo lilifungwa na baadhi ya maafisa wa usalama wenye bidii kupita kiasi kwa sababu zozote zile, basi wanapaswa kuwajibika.

Mamlaka ya Cameroon siku ya Ijumaa ililaumu tukio hilo la kuua kwa kile walichosema ni wimbi kubwa la mashabiki wasio na tiketi waliofika kwa kuchelewa kwenye mchezo uliohusisha timu mwenyeji na kujaribu kuingia kwa nguvu ili kuepusha ukaguzi wa usalama na uchunguzi wa COVID-19.

Nasseri Paul Bea, gavana wa jimbo la kati la Cameroon ambako Olembe ipo, anasema serikali itawasaidia waathiriwa wa mkanyagano huo baada ya mashindano hayo kumalizika. Anasema watu wanaohudhuria mechi za soka wakati wa AFCON wanapaswa kuacha tabia zisizo za kiungwana kama vile kuruka ukuta ili kuingia viwanjani.

Bea anasema tunatoa wito kwa watu hawa kufuata na kuheshimu taasisi, waweze kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa Cameroon haiwakilishi picha mbaya kwa kuwa wazalendo na kuwajibika sana. Isijirudie tena. Wacameroon wanapaswa kuweka akilini mwao kwamba kilichotokea Olembe kisitokee tena.

Bea alisema baadhi ya mawaziri wa serikali, maafisa wakuu wa serikali na watu wenye mapenzi mema wamekuwa wakitoa msaada wa kifedha kwa waathiriwa kwa mshikamano na jimbo la Cameroon.

Baada ya ajali hiyo Shirikisho la Soka barani Afrika lilisimamisha mechi za AFCON katika uwanja wa Olembe hadi hapo itakapotangazwa tena.

Cameroon ni mwenyeji wa AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka 50. Michuano hiyo, ambayo ni tukio kuu la kandanda barani humo, ilipangwa awali mwaka 2019. Shirikisho hilo liliiondoa Cameroon mwaka huo kwa sababu viwanja havikuwa tayari.

Mashindano ambayo yatafikia kilele Februari 6 na yalianza Januari 9.

XS
SM
MD
LG