Mcheza Gofu wa kulipwa Marekani, Tiger Woods, amepata ajali mbaya ya gari Jumanne kulingana na idara ya polisi ya kaunti ya Los Angeles nchini Marekani.
Gari la Woods limeripotiwa kupinduka mara kadhaa karibu na mji wa Ranchos Palos Verdes kwenye jimbo la California ambapo Woods alitolewa kutoka kwenye gari iliyoharibika vibaya. Picha za video katika eneo la ajali zinaonesha gari katika upande aliokuwa Woods limetumbukia kwenye shimo huku likiwa limeharibika vibaya. Vipande vya gari vilionekana karibu na mabaki ya mahala gari lilipotumbukia.
Woods alipelekwa katika kituo cha matibabu cha UCLA, mahala ambapo anapatiwa matibabu kwa majeraha, na imeripotiwa kuwa alikuwa peke yake ndani ya gari hilo. Ofisi ya sheriff wa kaunti ya LA imesema majeraha ya Woods hayakuwa katika kiwango cha kutishia maisha.
Gazeti la Los Angeles Times, liliripoti kwamba Woods alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi na alipoteza udhibiti wa gari, alivuka njia panda ambayo inagawanya maeneo na kisha gari lake likapinduka mara kadhaa kabla ya kujikuta kwenye shimo.