Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 04:25

Somalia yapata uungwaji mkono katika kampeni ya kutaka kuondolewa kwa vikwazo vya silaha


Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akihutubia Kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Septemba 22, 2022. REUTERS/Mike Sega.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud akihutubia Kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Septemba 22, 2022. REUTERS/Mike Sega.

Somalia inapata uungwaji mkono kwa kampeni yake ya kutaka kuondolewa kwa vikwazo vya silaha baada ya Ethiopia kuungana na Uganda kuunga mkono hatua hiyo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kupiga kura mwezi Novemba kuhusu kurejesha marufuku hayo ya kiasi, ambayo Somalia inasema inapaswa kuondolewa ili iweze kupambana vyema na magaidi wa al-Shabab.

Uungwaji mkono wa Ethiopia ulikuja baada ya uvamizi wa nadra wa mwezi Julai wa wanamgambo wa Kiislamu nchini Ethiopia huku kukiwa na mashambulizi makubwa ya Somalia na washirika wake dhidi ya kundi hilo. Ahmed Mohamed anaripoti kutoka Mogadishu, Somalia na Sunday Shomari anaisoma ripoti kamili.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wanasema vikwazo vilivyodumu kwa miongo mitatu vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vinapaswa kuondolewa ili Somalia iweze kupambana vyema na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabab.

Viongozi hao wawili walitoa taarifa ya pamoja Septemba 30 huku kukiwa na mashambulizi ya wanajeshi wa Somalia na washirika wao.

Somalia ilitoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika mwezi Julai kuunga mkono kampeni yake ya kuondoa vikwazo, ambavyo ni pamoja na kupiga marufuku silaha za hali ya juu na magari ya kijeshi.

Shirika la utafiti wa usalama lenye makao yake nchini Somalia la Hiraal Institute, katika ripoti ya mwezi Februari, lilisema vikwazo vya silaha vinashindwa kuwazuia al-Shabab kusafirisha silaha ambazo vikosi vya serikali haviruhusiwi kununua.

Samira Gaid wa taasisi hiyo anasema uwezo wa Somalia ni mdogo kwa sababu inahitaji ruhusa kutoka kwa wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kununua baadhi ya silaha.

Licha ya vikwazo, vikosi vya Somalia na washirika wake vimekuwa vikipata mafanikio dhidi ya wanamgambo hao.

Vita vikali vya Rais wa Somalia Mohamud dhidi ya kundi la al-Shabab vimeshuhudia vijiji vingi vilivyokombolewa kutoka kwa wanamgambo hao katika wiki za hivi karibuni za mapigano makali.

Kundi hilo la kigaidi linasema limeingiza hasara kwa wanajeshi wa Somalia, ingawa takwimu za majeruhi hazijathibitishwa.

Mohamed Muse Matan anafundisha Siasa na uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Somalia. Anasema vikwazo hivyo vinamaanisha kuwa vikosi vya Somalia havina nguvu za kutosha kuwashinda wanamgambo hao.

Lakini Matan anakiri kuruhusu Somalia kupata silaha za hali ya juu bado ni hatari.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiwekea Somalia vikwazo vya silaha mwaka 1992 kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na ghasia za makundi.

Vikwazo hivyo viliondolewa kwa kiasi mwaka 2013 ili kusaidia vikosi vya usalama vya Somalia kukua na kupambana na wanamgambo hao wa Kiislamu.

Vikwazo vilivyosalia, ambavyo vinahitaji maombi ya silaha fulani fulani kuidhinishwa, vinapitishwa upya kila mwaka.

Wakati Somalia kwa miaka mingi imekuwa ikitoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo hivyo, Rais Mohamud amekuwa akifanya kampeni tangu alipochaguliwa mwezi Mei kuungwa mkono na majirani zake.

Mwezi Agosti, Mohamud na Rais wa Uganda Yoweri Museveni walitoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo hivyo wakati wa ziara ya Mohamud mjini Kampala.

Aliyekuwa naibu mkurugenzi wa kijasusi wa taifa la Somalia Abdisalam Guled anasema Somalia inahitaji silaha nzito nzito kama vile vifaru vya kivita na magari ya kubeba askari wenye silaha (APCs).

Wachambuzi wanasema uvamizi wa al-Shabab mwezi Julai katika jimbo la Somalia la Ethiopia, mojawapo ya matukio mabaya zaidi yaliyoripotiwa katika kumbukumbu za hivi karibuni ilikuwa ndio sababu kuu katika wito wa Waziri Mkuu Abiy wa kuondoa vikwazo.

Maafisa wa Ethiopia wanasema walizuia uvamizi huo, na kuua zaidi ya wanamgambo 800 wa Kiislamu. Lakini haiwezekani kuthibitisha takwimu za majeruhi moja kwa moja kwa sababu eneo hilo haliruhusiwi kwa waandishi wa habari.

atika kura ya mwisho ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuongezwa kwa marufuku hiyo Novemba 2021, Kenya ilikuwa miongoni mwa wanachama 13 wa baraza hilo walioidhinisha kurefushwa kwa marufuku hiyo kwa kiasi.

Huku kura ijayo ikiwa imesalia wiki chache tu, haijabainika iwapo Kenya itaunga mkono msukumo wa Somalia wa kutaka kuondolewa kwa vikwazo hivyo. Hakukuwa na majibu kwa maombi ya maoni kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya.

Hata kama Nairobi itaunga mkono hatua hiyo, Somalia itahitaji kuungwa mkono zaidi na baraza hilo ili vikwazo hivyo viondolewe.

XS
SM
MD
LG