Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:47

Serikali ya Sudan yalaumiwa kutokana na maafa katika maandamano


Watu wakiimba na kuandamana katika mitaa ya Sudan walipodai utawala wa kijeshi ukabidhi madaraka kwa raia mjini Khartoum, Sudan, Juni 30, 2019.
Watu wakiimba na kuandamana katika mitaa ya Sudan walipodai utawala wa kijeshi ukabidhi madaraka kwa raia mjini Khartoum, Sudan, Juni 30, 2019.

Serikali ya mpito ya Sudan imeshambuliwa baada ya vikosi vya usalama nchini humo kutumia risasi za moto Jumanne kuwatawanya watu waliofanya maadhimisho ya miaka miwili ya maandamano yanayounga mkono demokrasia, na kupelekea watu wawili kufariki dunia.

Juni 3, 2019, wanajeshi waliwafyatulia risasi waandamanaji wanaounga mkono demokrasia ambao walikuwa wamezunguka makao makuu ya jeshi mjini Khartoum, na kuua zaidi ya watu mia moja.

Jamaa wa waathirika walikusanyika karibu na makao makuu ya jeshi katika mji mkuu Jumanne ili kukumbuka wale waliouawa.

Amira Kabous, ni naibu kiongozi wa Familia za Mapinduzi ya Desemba, alihutubia waandamanaji alisema “katika njia panda hii ya kihistoria, wakati familia za waathirika zinajipanga, wananyoosha vidole kwa Mohamed Hamdan Daglo, mkuu wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, kwa kufanya mauaji ya Juni 2019. Wanamshtaki pia kwa unyanyasaji mwingi kabla na baada ya kutawanywa wale waandamanaji waliokuwa wamekaa”.

Saa chache baada ya mkutano wa Jumanne, vikosi vya usalama vilifyatua risasi za moto kutawanya waandamanaji waliosalia na kuua watu wawili. Darzeni kadhaa walijeruhiwa, na walioshuhudia wanasema wengi walikamatwa baada ya shambulio hilo.

Jeshi la Sudan lilikanusha uhusiano wowote kwa shambulio hilo na kusema halikutoa maagizo ya kutumia risasi za moto. Jeshi limesema litafungua uchunguzi.

Siku ya Jumatano, ofisi ya Waziri Mkuu Abdallah Hamdok ilisema Hamdok alikutana na majenerali, wakuu wa wizara za Mambo ya Ndani na Ulinzi na maafisa wengine kujadili tukio la Jumanne.

Katika taarifa iliyotolewa, Hamdok alielezea masikitiko ya serikali ya mpito kwa tukio la umwagaji damu na utumiaji wa nguvu kupita kiasi na akalitaka jeshi na mfumo wa sheria kusaidia katika uchunguzi.

Ubalozi wa Marekani ulielezea mshtuko wake na kulaani utumiaji wa risasi za moto, na kuitaka mamlaka ya mpito ichunguze shambulio hilo kikamilifu.

Maafisa wengi na vyama ambavyo vina majukumu katika serikali ya mpito waliwataka maafisa wakuu kujiuzulu ikiwa mamlaka itashindwa kutaja na kushtaki askari waliofyatua risasi.

Serikali ya mpito iliingia madarakani mwaka 2019 baada ya majenerali kumwondoa madarakani rais wa muda mrefu Omar al-Bashir kufuatia maandamano ya miezi kadhaa dhidi ya utawala wake.

Mnamo mwezi Agosti, viongozi wa maandamano na majenerali walitia saini makubaliano ya kugawana madaraka.

Kulingana na makubaliano hayo, majenerali wa jeshi wanapaswa kukabidhi madaraka kwa kiongozi wa kiraia aliyetajwa na viongozi wa maandamano baadaye mwezi huu.

Juni 3 ni maadhimisho ya miaka miwili ya mauaji hayo. Waandamanaji wanaounga mkono demokrasia wametangaza tarehe hiyo kama tarehe ya mwisho kwa mamlaka ya mpito kuanza kuwashtaki wale waliosababisha tukio hilo na mauaji ya watu hao Jumanne.

XS
SM
MD
LG