Video inayoonekana kuonyesha vikosi vya usalama vya Msumbiji vikiwatesa na pengine kuuwa wanamgambo imepelekea wito wa uchunguzi na huku maafisa wa serikali wakikanusha madai hayo.
Amnesty International ilipata video tano na picha tatu inazosema zilipigwa katika mkoa ulio na ghasia wa Cabo Delgado. Picha hizo zimeangaliwa kwa makini na Maabara ya Ushahidi ya mizozo ya shirika hilo ambao wanaamini ni za kweli na imechukuliwa katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2020.
Brian Castner, mshauri mwandamizi wa migogoro wa Amnesty International wa operesheni za silaha na jeshi, aliiambia VOA kwamba video moja inaonyesha wanajeshi hao wakishangilia wakati wafungwa wanapigwa mateke na kupigwa kwa vitako vya bunduki.
Anasema katika tukio mojawapo mmoja wa wanajeshi alimkata sikio mmoja wa wafungwa hao na anamkabidhi huku watu wakishangilia, Katika kesi nyingine, Castner anasema wanatishia kumwasha moto mfungwa akingali hai.
Siku ya Alhamisi, Omar Saranga, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Msumbiji, alisema kuwa picha hizo zinapaswa kutazamwa kwa mashaka. Sare za kijeshi kwenye video hizi na picha hazipaswi kuaminiwa moja kwa moja na sio sahihi, aliwaambia waandishi wa habari huko Maputo.
Saranga alisema kuwa vikundi vyenye msimamo mkali na waasi wanatafuta kudhalilisha vikosi vya usalama kwa kuvaa mavazi yao.